Habari Mseto

Wafanyakazi waliouza umeme wa Kenya Power kwa bei nafuu wafutwa

July 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini, Kenya Power (KP)imefichua imewafuta kazi wafanyakazi wake 13 waliwauzia wateja umeme wa luku, maarufu kama tokens, wa thamani ya Sh35 milioni kwa bei nafuu bila idhini yake.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Jared Othieno Jumatano aliwaambia maseneta kwamba sakata hiyo iliwahusu jumla ya wateja 3,500 ambao waliuziwa umeme huo kati ya Januari 2018 na Februari 2019.

“Uchunguzi wetu uligundua kuwa wateja walioshiriki katika sakata hii walinunua ‘token’ hizo wakifahamu kuwa hazikuwa zimehalalishwa rasmi ya kampuni yetu. Na tumewaadhibu wafanyakazi wetu waliofanikisha sakata hiyo kuwa kuwaachisha kazi,” Mhandisi Othieno akaambia kamati ya seneti kuhusu Kawi inayoongozwa na Seneta Ephraim Maina.

Afisa huyo alisema sakata hiyo ilichangia kampuni hiyo kupata hasara na ndio maana imeanza kufidia hasara hiyo kutoka kwa wateja husika kupitia mfumo huo huo wa ununuzi “token”.

Mhandisi Othieno alisema kuwa sakata hiyo ilianza pale walaghai fulani walipoweka matangazo kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanauza ‘token’ kwa bei nafuu, wakidai ni maajenti wa KP.

“Kwa mfano, mteja aliyenunua ‘token’ ya thamani ya Sh1,000 aliishia kupewa umeme wa thamani ya Sh2,000. Hii ina maana kuwa wauzaji na wananunuzi walifaidi huku KP ikipoteza,” akawaambia maseneta hao.

Mkurugenzi huo alisema ni wateja walionunua “token’ hizo kinyume cha sheria pamoja na wengine ambao waliunganishiwa stima kwa mkopo chini ya mradi wa usambazaji wa stima mashinani (Last Mile) ndio wamekuwa wakitozwa ada za juu za stima.

“Wateja kama hawa na wale waliofaidi kutokana na mradi wa Last Mile ndio wamekuwa wakipata kipengee kwa jina “Total Debt” katika bili zao au risiti za “token” wanazonunua,” Bw Othieno akawambia wanachama wa kamati hiyo.

Afisa huyo ambaye aliandamana na Waziri Msaidizi wa Kawi Simon Kachapin, alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kujibu swali la Seneta wa Vihiga George Khaniri kuhusu sababu ya kupanda kwa gharama ya malipo ya bili za stima.

Bw Khaniri pia alitaka kampuni hiyo ielezee ni kwa nini baadhi ya wateja wamekuwa wakilalamika kuwa wao hupata kiwango kidogo cha umeme kwa kiwango sawa cha fedha.

“Kwa nini kwa mfano, mteja akinunua ‘token’ ya Sh1000 anapata kiwango cha chini cha umeme kuliko ilivyokuwa zamani ilhali sera ya serikali ni kupunguza bei ya stima,” akauliza wiki jana.

Lakini maseneta Ladema Ole Kina (Narok), Ochilo Ayacko (Migori) na Mary Seneta (Seneta Maalum) walisema baadhi ya wananchi hawakufahamu wa “Last Mile” ulikuwa ni mkopo wa kulipiwa.

“Hii ndio maana wakazi wa mashambani wanalalamika wanapoletewa bili za juu. Walidhani mradi huo ambapo waliunganishiwa stima ulikuwa ni ruzuku,” akasema Bw Ole Kina.

Seneta huyo aliitaka KP kutoa uhamasisho kwa wateja wake kuhusu ada za stima ili kuzua hali ambapo baadhi yao wanadhani wanatozwa ada za juu bila sababu.