Habari MsetoSiasa

Wafuasi wa Ruto waonyesha dalili za kufufua URP

April 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ERIC WAINAINA

WAFUASI wa Naibu Rais William Ruto, Jumapili walionyesha ishara ya kufufua chama chake cha zamani cha United Republic Party (URP) na huenda akakitumia kuwania urais 2022 kama Chama cha Jubilee kitasambaratika.

Vijana waliovaa fulana za rangi ya manjano ambayo ilikuwa rangi rasmi ya URP kabla kilipovunjwa kuunda Jubilee, walijitokeza kwa wingi kumlaki Naibu Rais alipozuru eneo la Banana, Kaunti ya Kiambu.

Wadadisi wanasema uamuzi wao kuvaa mavazi ya manjano huenda ukawa ni ishara ya mgawanyiko ulio katika Chama cha Jubilee kati ya wandani wa Dkt Ruto na Rais Uhuru Kenyatta.

Naibu Rais alikuwa amehudhuria ibada katika Kanisa Katoliki la St Martin, eneo la Karuri ambapo baadhi ya viongozi wa eneo hilo walieleza wazi nia yao ya kuendelea kumfanyia kampeni kinyume na maagizo ya Rais aliyetaka siasa za 2022 zikomeshwe.

Zaidi ya hayo, wao ndio walikusanya vijana waliovaa mavazi hayo yaliyokuwa na picha za Dkt Ruto na maandishi #teamWSR.

Huku wakiwika maneno ya kumsifu Naibu Rais, vijana hao pia waliandamana wakiwa wamebeba bango kubwa lenye picha ya Dkt Ruto na maandishi ‘our choice 2022’ (chaguo letu 2022) na mabango mengine ya kampeni za urais.

Dkt Ruto hudai Kiongozi wa Upinzani, Bw Raila Odinga anapanga kumfurusha katika Jubilee. Wandani wake hulalamika kwamba kuna njama ya kubadilisha makubaliano yaliyokuwepo kati yake na Rais kuhusu urithi wa mamlaka ifikapo 2022.

Ingawa duru zilisema kuna uwezekano mkubwa Naibu Rais hakujua kuhusu vijana hao, mavazi yao ya manjano ndio yalivutia hisia tele za kisiasa.

Kabla kusajiliwa kwa Chama cha Jubilee kilichotumiwa na Rais na naibu wake 2017 kuwania urais, kulikuwa na Muungano wa Jubilee ambapo vyama vya The National Alliance (TNA) kilichokuwa cha Rais Kenyatta na URP cha Dkt Ruto vilikuwa washirika.

Nembo ya Chama cha Jubilee ina rangi nyekundu iliyokuwa ya TNA, manjano ya URP na nyeusi.

Akiwa Karuri, Dkt Ruto alikuwa na wandani wake wakiwemo Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, mwenzake wa Kajiado, Bw Joseph ole Lenku, Wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Jude Njomo (Kiambu Mjini), Alice Wahome (Kandara) na Cate Waruguru (Laikipia) miongoni mwa wengine.

Kikosi hicho ambacho hutambulika sana kama ‘team tanga tanga’ kilikashifu kikundi kingine cha viongozi wanaoegemea upande wa Rais Kenyatta na ajenda zake, hasa kuhusu mwafaka wa Rais na Bw Odinga na vita dhidi ya ufisadi.

Wamekuwa wakidai ajenda hizo zinalenga kuzima maazimio ya Dkt Ruto kushinda urais ifikapo 2022.

Rais amekuwa akisisitiza kwamba viongozi wanafaa kukomesha siasa na badala yake watilie maanani hitaji la kutekeleza mipango ya maendeleo na kuunga mkono juhudi zake za kupambana na ufisadi.