Habari Mseto

Wakalenjin waitaka Mlima Kenya kuheshimu mkataba na kuunga Ruto 2022

August 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA OSCAR KAKAI

Baraza la wazee wa jamii ya Wakalenjin, maarufu kama Myoot, limewataka wenzao wa eneo la Mlima Kenya, kuheshimu ahadi yao ya kuunga mkono Naibu Rais Bw William Ruto kwenye uchaguzi wa 2022.

Wazee hao walisisitiza kuwa licha ya Bw Ruto mwenyewe kusema hadai lolote la kisiasa kutoka kwa wakazi wa eneo la Mlima Kenya au jamii nyingine, wazee wa Wakalenjin wanajua bado kuna deni.

Walisema wazee kutoka jamii hizo mbili walikutana mjini Eldoret na Nakuru miaka sita iliyopita na kukubaliana kuwa eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono Bw Ruto 2022.

Akiongea na wanahabari mjini Kapenguria, mwenyekiti wa baraza hilo Bw James Lukwo alisema wazee kutoka jamii hizo mbili walikutana mara mbili na kukubaliana kuwa itakuwa zamu ya William Ruto baada ya Uhuru Kenyatta kumaliza kipindi chake.

“Kama jamii, tunataka wenzetu kutoka eneo la Kati kujitokeza wazi na kutueleza ukweli. Tunataka kujua ikiwa wametutupa. Wanafaa kutangaza msimamo wao mapema. Tunahusika na kujali kama wazee kwa sababu tunataka amani,” alisema.

Waliwataka wazee wa baraza la jamii ya Wakikuyu kuacha kuwaruka.

“Wanafaa kuwa wanaume kamili na kutueleza ikiwa wataunga kijana wetu 2022,” alisema Bw Lukwo.

“Tunafaa kukutana na kujadili suala hili kwa sababu tunahitaji amani na maendeleo. Tuko na wimbo moja wa kumuunga mkono Naibu wa Rais lakini sio wimbo mwingine,” alisema Bw Lukwo.

Aliongeza kuwa chama cha Jubilee kinafaa kuendelea kuungana.

Ingawa Bw Ruto amekuwa akipinga mjadala kuhusu madeni ya kisiasa ya 2022 mjadala huo bado unaendelea.