Wakati wa kumtimua Kiunjuri ni sasa, wabunge wamwambia Rais
Na CHARLES WASONGA
MAPEMA Jumatano wabunge wa North Rift walimtaka Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri kujiuzulu kwa kusimamia wizara hiyo visivyo haswa kuhusiana na suala la uagizaji mahindi kutoka nje.
Wakiongozwa na Mbunge wa Cherangany Joshua Kuttuny wabunge hao pia walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi Bw Kiunjuri la sivyo wawasilishe bungeni hoja ya kumwondoa mamlakani.
Viongozi hao walimshtumu Waziri huyo kwa kuamuru Hazina ya Kitaifa ilipe kampuni kwa jina Commodities House Ltd kitita cha Sh1.8 bilioni ili ilete mahindi nchini kutoka mataifa ya mbali kama vile Mexico
Kwenye kikao na wanahabari katika majiengo ya bunge Kuttuny ambaye alikuwa amendamana na wenzake Silas Tiren (Moiben), Alfred Keter (Nandi Hill) na Caleb Amisi (Saboti) walidai kuwa pesa hizo zilitolewa kinyume cha sheria kutoka akaunti maalum ya Bodi ya Hifadhi Maalum ya Chakula Nchini (SFRB) na kulipwa kwa kampuni hiyo.
Wabunge hao sasa wanataka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ADPP) kuchunguza malipo hayo.
“Tumechukua hatua hii kwa sababu ni wazi kuwa malipo hayo yalitolewa cha sehemu ya 4 (3), sehemu ya 5 (1), (C), 8 (j) 14 (1 na 2) ya Sheria ya Usimamizi wa Pesa za Umma na Kanuni za Hazina ya Uhafadhi Maalum wa Chakula (SFRB) ya mwaka wa 2015,” akasema Bw Kuttuny.
Wabunge ambao pia walijumuisha Dkt Robert Pukose (Endebess) na Marwa Kitayama (Kuria Mashariki) walisema pesa hizo zilipwa bila idhini ya bodi ya SFRB.
“Tunajua kuwa SFRB imekuwa ikilipa malimbikizi ya madeni lakini tuma uhakikisha kwamba haikuidhinisha malipo kwa kampuni hii ya Commodities House ltd ambayo shughuli yake kuu huwa ni kuagizaji mahindi kutoka nje ya Kenya,” akasema Bw Keter.
Lakini akijibu madai ya wabunge hao, Bw Kiunjuri alisema kuwa pesa hizo (Sh1.8 bilioni) zililipwa Commodities House Ltd ni sehemu ya Sh3.6 bilioni ambazo inadai serikali.
“Ningependa kutoa ufafanuzi kuwa pesa hizo zilikuwa za kulipia deni ambalo tunadaiwa na kampuni hiyo miongoni mwa kampuni nyinginezo. Hizo sio pesa za kuagiza mahindi kutoka Mexico inavyodai na watu wengine,” akasema alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo.
Hata hivyo, Waziri Kiunjuri alishindwa kuwaeleza wabunge hao ni kwamba ni kampuni hiyo pekee iliyolipwa ilhali kuna kampuni nyingi pamoja na zile za usagaji unga ambazo zinadai Wizara yake kiasi kikubwa cha pesa.