Wakazi wafokewa kuficha Al Shabaab msituni Boni
NA KALUME KAZUNGU
WAKAZI wa maeneo ambako kumekuwa kukitekelezwa mashambulizi na mauaji ya mara kwa mara na magaidi wa Al-Shabaab kaunti ya Lamu na sehemu za mpakani mwa Lamu na Somalia wamekashifiwa kwa kuwaficha magaidi wanaoendeleza mashambulizi hayo.
Afisa wa operesheni ya usalama inayoendelezwa kwenye msitu wa Boni ambaye pia ni Kamishna wa Lamu, Joseph Kanyiri, anasema wakazi kwenye maeneo husika wamekuwa wakificha taarifa kuhusu kuonekana kwa magaidi kwenye maeneo yao ilhali wengine wakiwaficha magaidi hao kwenye nyumba zao.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Jumatano, Bw Kanyiri alisema hatua hiyo ni kizingiti kikuu katika kukabiliana na kuwamaliza Al-Shabaab ndani ya msitu wa Boni.
Alisema hulka ya wakazi ya kushirikiana na wahalifu pia inalemaza juhudi za kuafikiwa kwa amani na utulivu kaunti ya Lamu.
Alisema inasikitisha kwamba baadhi ya wakazi hasa kwenye sehemu za Bar’goni, Bodhei, Milihoi na maeneo mengine ambayo Al-Shabaab wamekuwa wakishambulia wamekuwa wakijidai kutokuwa na ufahamu na wale wanaoendeleza mashambulizi hayo.
Alisema idara ya usalama iko na ripoti kuwahusu majasusi na wafadhili wa Al-Shabaab miongoni mwa jamii za maeneo husika.
Alitaja shambulizi la hivi majuzi dhidi ya gari la maafisa wa jeshi (KDF) eneo la Kwa Omollo kwenye barabara kuu ya Bodhei kuelekea Bar’goni kuwa dhihirisho tosha kwamba jamii imekuwa ikihusika moja kwa moja katika kuwasaidia Al-Shabaab kutekeleza mashambulizi.
Jumla ya maafisa sita wa KDF waliuawa ilhali wengine watano wakijeruhiwa vibaya wakati wa shambulizi hilo la kilipuzi cha kutegwa ardhini.
Bw Kanyiri alitoa tahadhari kwa jamii kujiepusha kushirikiana na Al-Shabaab.
“Ukitafakari jinsi shambulizi hilo lilivyotekelezwa utatambua bayana kwamba jamii inahusika moja kwa moja. Wao ndio wanaopeana habari punde gari la KDF au polisi linapopita maeneo husika ili kuwapa nafasi Al-Shabaab kuandaa mashambulizi yao.
Hayo ni mambo yasiyofaa. Ni vyema jamii kushirikiana na walinda usalama. Watoe ripoti kwa walinda usalama wetu ili kudhibiti usalama wa eneo hili. Ikiwa hakuna ushirikiano basi itakuwa vigumu kukabiliana na kumaliza vita dhidi ya Al-Shabaab Lamu,” akasema Bw Kanyiri.