Wakazi wafurahia biashara ya mafuta ndani ya Bahari Hindi
NA KALUME KAZUNGU
WAUZAJI mafuta ya petroli, diseli na gesi ndani ya Bahari Hindi, Kaunti ya Lamu wamekiri kupata kivuno kutokana na idadi ndogo ya wanabiashara ambao wamejitolea kuwekeza kwenye biashara hiyo.
Wafanyabiashara wa petroli, diseli na gesi katika kisiwa cha Lamu hawaruhusiwi kuendeleza biashara hiyo ndani ya mji huo na badala yake wanatakiwa kuweka vituo vyao vya mafuta ndani ya Bahari Hindi.
Sababu kuu ya kaunti kuafikia marufuku hiyo ni kwamba mji wa kale wa Lamu ni mdogo.
Isitoshe, nyumba nyingi ziko pamoja pamoja, hatua ambayo inaleta ugumu kwa magari ya kuzima moto kuhudumu ndani ya mji endapo mikasa ya moto itazuka.
Kufuatia ughali wa kuwekeza vituo vya mafuta ndani ya Bahari Hindi, ni wafanyabiashara wachache pekee ambao wanaendelea biashara hiyo.
Katika kisiwa cha Lamu ambapo zaidi ya wakazi 10,000 wanaishi, vituo vitano pekee vya mafuta ndivyo vinavyohudumia idadi hiyo kubwa ya wakazi.
Utafiti uliofanywa na Taifa Leo juma hili ulibaini kwamba biashara ya vituo vya mafutya ndani ya bahari ni miongoni mwa uwekezaji unaofanya vyema zaidi kwenye mji wa Lamu.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na wanahabari walisema wanahudumia mamia ya wateja kila siku, hatua ambayo imewafanya kuvuna faida kubwa.
Mmoja wa wamiliki wa biashara hizo, Bw Omar Abdalla alisema licha ya kupata ugumu katika kuanzisha na kuendeleza kituo vya mafuta baharini, bado wanapata faida ambayo inawawezeka kuiendeleza biashara hiyo.
“Mwanzo wa kubuni kituo cha mafuta baharini huwa ndio mgumu lakini kuendeleza biashara hiyo si shida. Utahitajika kusafirisha mafuta kutoka Mombasa hadi Lamu.
Kisha utahitajika kuyavukisha hadi kwenye kituo chako cha mafuta ndani ya bahari. Zote hizo ni gharama lakini licha ya yote bado tunapata faida baada ya kuuza mafuta hayo,” akasema Bw Abdalla.
Mmoja wa wahudumu wa kituo cha mafuta ndani ya Bahari Hindi, Crasmy Wanje alikiri kuhudumia hadi wateja 3000 kwa siku.
“Wateja wangu wengi ni wahudumu wa boti, waendeshaji pikipiki na hata watalii wanaozuru eneo hili wakitumia boti zao za kisasa. Mimi huuza mafuta na kupata hadi Sh 200,000 kwa siku.
Biashara ya mafuta ndani ya Bahari inafanya vyema kwani hatuna ushindani wa kibiashara hapa,” akasema Bw Wanje.