• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 AM
Wakazi wamtaka Obama akubali chuo kikuu kipewe jina lake

Wakazi wamtaka Obama akubali chuo kikuu kipewe jina lake

Na Victor Raballa

WAKAZI wa K’Ogelo wanamtaka aliyekuwa rais wa Amerika, Barack Obama, akubali hadharani chuo kikuu kinachopangiwa kujengwa eneo hilo kipewe jina lake.

Wakazi tayari wametenga ekari 24 za ardhi kwa ujenzi wa bewa kuu la chuo hicho kilichopendekezwa katika kijiji cha Nyang’oma K’Ogelo.

Chuo hicho ambacho kimependekezwa kiitwe Chuo Kikuu cha Barack Obama cha Uongozi na Ufundi, ni miongoni mwa matakwa sita ambayo yamepangiwa kuwasilishwa na wakazi kwa Bw Obama atakapozuru eneo hilo leo.

Msemaji wa jamii, Bw Nicholas Rajula, alisema mashauriano yanaendelea ili Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Siaya, ambacho kwa sasa kinashirikiana na Chuo Kikuu cha Maseno, kisimamie chuo hicho kikuu kipya.

Gavana wa Siaya, Bw Cornel Rasanga, alieleza matumaini yake kwamba chuo hicho kikifunguliwa kitaamsha kijiji hicho ambacho husisimka tu wakati Obama anapozuru.

Mbali na hayo, alisema kitasaidia kutoa mafunzo maalumu yatakayoimarisha maendeleo ya kaunti 14 zinazozunguka Ziwa Victoria kukiwa na lengo moja la kupambana na umasikini.

Katika hafla ya awali, Bw Rasanga alisema kuna umuhimu wa kuanzisha masomo kama vile kuhusu unyunyizaji maji mashambani, matibabu ya magonjwa yanayokumba maeneo ya ziwani na vile vile sheria kwani Bw Obama ni wakili.

You can share this post!

Wataalamu nao waunga mkono Katiba igeuzwe

MIGORI: Wafanyakazi hewa wamekuwa wakinyonya Sh10m kila...

adminleo