INFOTRAK: Wakenya wanataka IEBC ivunjwe
Na CHARLES WASONGA
IDADI kubwa ya Wakenya inataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ivunjwe.
Matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa Jumapili yanaonyesha kuwa asilimia 53 ya Wakenya wamekosa imani ya tume hiyo na wataka maafisa wote wanaoisimamia wafunganye virago, ili tume hiyo ibuniwe upya.
Kulingana na Afisa Mkuu wa shirika la Infotrak, Bi Angela Ambitho, ni chini ya robo (asilimia 21 pekee) ya Wekenya wanaosema kuwa tume hiyo inafaa kuwepo.
Utafiti huo uliowahusisha watu 1,538 waliohojiwa, ulionyesha kuwa sababu kubwa zinazowafanya watu wasiwe na imani na IEBC, ni migogoro ya uongozi, ufisadi na kutosuluhishwa kwa masuala yaliyoibuliwa na aliyekuwa kamishna Dkt Roselyne Akombe.
Utafiti wa jana ulifanywa karibu mwaka mmoja baada ya utafiti mwingine mwaka jana kuonyesha Wakenya hawakuwa na imani na tume hiyo.
Kwenye utafiti huo wa Septemba 2017, Infotrak iligundua kuwa asilimia 52.4 ya waliohojiwa hawakuwa na imani na tume, ambapo asilimia 43.8 walitaka Afisa Mkuu Mtendaji aliyesimamishwa kazi, Ezra Chiloba na mameneja wengine muhimu waliohusika na usimamizi wa uchaguzi wajiuzulu.
Utafiti ambao matokeo yake yalitangazwa jana, ulifanywa kati ya Agosti 20 na 23 katika kaunti 26.
Kuhusu mkondo ambao nchi inaelekea, Wakenya waligawanyi nusu kwa nusu, kundi moja likisema inaelekea pabaya, huku jingine likisema iko katika barabara nzuri.
Asilimia 43 walisema tunaelekea kuzuri, lakini asilimia 40 hawakukubalia na kauli hiyo.
Sehemu kubwa ya wanaoamini kuwa nchi iko kwenye njia imara wanasema ni kutokana na utulivu unaoshuhudiwa tangu kusalimiana kwa mikono kwa Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.