Habari Mseto

Walimu walia kukosa matibabu NHIF ikikosa kuwafaa

Na ELIZABETH OJINA June 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WALIMU katika Kaunti ya Kisumu wameelezea wasiwasi wao kuhusu kucheleweshwa kutolewa kwa fedha za Bima ya Afya Nchini (NHIF).

Hali hii imewalazimu walimu kulipa kutoka mifukoni mwao ili kugharamia matibabu yao binafsi na ya wanaowategemea.

Mamia ya walimu wamenyimwa matibabu hospitalini kwa sababu bima hiyo haiwezi ikaidhinisha malipo.

Katibu Mkuu wa Kuppet Kaunti ya Kisumu, Zablon Awange, amekashifu hali ya walimu kuhangaishwa kwa kukosa kutoa fedha za kushughulikia matibabu.

“Serikali bado haijatoa fedha za NHIF za kushughulikia walimu. Tunaitaka serikali itoe pesa zote za NHIF ili kuwezesha wagonjwa kupata huduma,” alisema Bw Awange.

Serikali hivi majuzi ilianzisha mageuzi kuhusu bima ya afya ili kukaribisha Hazina ya Afya ya Jamii (SHIF) inayodhamiriwa kuwezesha Wakenya kunufaika kutokana na mpango wa Afya kwa wote.

Hata hivyo, juhudi hizo za kulainisha huduma ya Afya kwa umma imesababisha changamoto za kifedha.

Mwaka uliopita, Hazina Kuu ilitoa Sh5.1 bilioni kufadhili robo ya kwanza ya bajeti katika mwaka wa kifedha, 2023/2024.