Walimu wastaafu kusubiri malipo yao kwa muda zaidi
Na JOSEPH OPENDA
WALIMU 52,000 waliostaafu mnamo 1997 wamepata pigo kwenye kesi waliyowasilisha mahakamani wakitaka Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) iwalipe pensheni na malimbikizi ya mishahara ya Sh43 bilioni baada ya tume hiyo kupinga kiwango hicho ikisema kiliafikiwa visivyo.
Kulingana na TSC, fedha zinazofaa kulipwa ni Sh17 bilioni wala si Sh43 bilioni jinsi wanavyodai walimu hao wa waliostaafu.
TSC imewasilisha ombi katika mahakama kuu ya Nakuru ikitaka kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa na jopo la majaji watatu au zaidi watakaoteuliwa na Jaji Mkuu David Maraga, ili kutoa ufafanuzi kuhusu kiwango kamili cha fedha kinachofaa kulipwa.
Kupitia wakili wao Lawrence Karanja, TSC inadai kwamba suala hilo ni la umma na linafaa kushughulikiwa kwa makini ili kuzuia kosa lolote wakati wa kutoa uamuzi.
“Tunaiomba mahakama kudhibitisha kwamba suala lililoibuliwa linazua maswali ya kisheria na mara moja iwasilishe kesi hii kwa Jaji Mkuu ili ateue jopo la majaji watatu au zaidi kulingana na kifungu 165 ibara ya nne ya katiba kusikiza na kuiamua,” ikasema sehemu ya ombi la Bw Karanja.
Hata hivyo, ombi hilo lililofaa kusikizwa Alhamisi pamoja na mengine yaliyowasilishwa na wahusika wengine kwenye kesi, yalikosa kusikizwa mahakama ilipoelezwa kwamba baadhi ya wahusika hawakuwa wameyawasilisha maombi yao.
Bw Karanja akiwa moja wao, alisema kwamba hakuwa amejibu baadhi ya madai yaliyowasilishwa dhidi ya mteja wake ndipo Jaji Janet Mulwa akampa siku 15 za kukamilisha kazi hiyo. Hata hivyo uamuzi huo ulipingwa na wakili wa walimu hao wastaafu Dominic Kimatta.
Walimu hao walipata ushindi mara mbili mahakama ya juu ilipotupilia mbali pingamizi kutoka kwa ofisi ya mwanasheria mkuu na TSC na kuagiza walimu hao walipwe pesa zao.
Hata hivyo, kulipwa kwao bado kumekuwa kitendawili huku TSC ikijikokota na kusema kwamba inaendelea kutathmini na kuidhinisha orodha kamili na kiasi cha fedha kila moja wao anafaa kupokea.