• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Waliochochea ghasia katika hafla ya Ruto motoni

Waliochochea ghasia katika hafla ya Ruto motoni

JOSEPH WANGUI NA NICHOLA S KOMU

KAMATAKAMATA yanukia katika Kaunti ya Nyeri dhidi ya viongozi na makundi ya vijana yaliyozua ghasia na makabiliano kwenye mkutano wa kuchangisha fedha uliohudhuriwa na Naibu Rais Dkt William Ruto siku ya Jumapili.

Polisi tayari wanamsaka Naibu Spika wa bunge la kaunti hiyo Samuel Kariuki ambaye alinaswa kwenye kanda ya video akiwapiga vijana waliodaiwa kuwa wafuasi wa kundi la Kieleweke wakati wa mchango huo ulioandaliwa katika kanisa la Giakanga AIPCA.

Haya yanajiri huku wawekezaji na wafanyabiashara wakitoa wito kwa serikali kupiga marufuku mikutano yote ya kisiasa katika kaunti ya Nyeri.

Vilevile wametoa wito wa kunyakwa kwa wanasiasa wanaowachochea wafuasi wao kuzua ghasia ambazo zimeongezeka kwenye mikutano ya kisiasa eneo hilo.

Akithibitisha nia ya kukamatwa kwa wanasiasa waliohusika na tafrani hiyo, Kamishina wa Ukanda wa Kati, Wilfred Nyagwanga alisema oparesheni ya kumnyaka Bw Kariuki inaendelezwa hadi kaunti ya Kilifi ambako anahudhuria warsha.

“Diwani huyo alisafiri kwa ndege hadi Pwani Jumapili jioni na tunamwomba ajisalimishe au tumkamate kwa lazima. Amri ya kumatwa kwake tayari imetolewa,” akasema Bw Nyagwanga.

Akigusia ghasia hizo, afisa huyo wa utawala alisema maafisa wa usalama watakuwa ange kuhakikisha wanasiasa wachochezi wanaotumia makundi ya vijana kuvuruga mikutano ya viongozi wengine wanakamatwa.

“Wale waliobeba silaha kwenye mkutano huo watakabiliwa vilivyo kulingana na sheria. Mtu yeyote aliyeshiriki vurugu hizo pia hatasazwa. Iwapo kiongozi yeyote hafurahii mkutano unaofanyika, basi anafaa kutoshiriki badala ya kutumia vijana kuzua taharuki,” akasema Bw Nyagwanga.

Katika video hiyo inayoendelea kusambaa, Bw Kariuki alionekana akiwatandika vijana hao kwa bakora kisha kuwakabidhi kwa polisi wasio na sare waliokuwa wakisubiri kwenye gari aina ya Land Rover.

Matamshi makali ya kamishna huyo yanajiri baada ya mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu kulalamika kwamba polisi waliyapa makundi ya vijana yaliyojihami kwa bakora jukumu la kulinda usalama kwenye mkutano huo.

Mbunge huyo wa mrengo wa Kieleweke alisema polisi hao walitekeleza majukumu yao kwa mapendeleo na kutoa wito wa kuhamishwa kwa wakuu wote wa polisi katika eneobunge lake.

Kulingana naye, polisi walitazama tu kwa furaha jinsi ambavyo vijana wanaopinga siasa za Naibu Rais walivyokuwa wakitandikwa na wale wanaorindima ngoma ya mrengo wa Tangatanga wakiongozwa na diwani huyo.

“Kulikuwa na zaidi ya polisi 40 na waliacha makundi ya vijana hatari kuchukua jukumu la kutoa ulinzi. Nimewaandikia barua Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, Katibu katika wizara hiyo Karanja Kibicho na kumnakilia kamishna wa kaunti.

“Ni wazi kuwa polisi hao waliegemea mrengo wa Tangatanga,” akasema Bw Ngunjiri akifichua kwamba kulikuwa pia na mpango wa kumwadhibu na kuharibu gari lake.

“Kulikuwa na njama ya kunisawiri pamoja na wafuasi wangu kama wanaopenda fujo. Pia walikuwa na njama ya kuhakikisha ninavamiwa na kuangushiwa kipigo,” akasema.

Mfanyabiashara na mwanachama wa Muungano wa Wafanyabiashara mjini Nyeri Thuo Mathenge alisema wanaendelea kupata hasara kubwa kutokana na ubabe wa kisiasa kati ya Bw Ngunjiri na Naibu Rais eneo la Nyeri.

You can share this post!

Afrika yashauriwa kukoma kuwanyima vijana nafasi maishani

USIU-A yaifunza Sailors jinsi ya kucheza magongo

adminleo