Waluke amwomba Tuju msamaha
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Sirisia, John Waluke ameomba msamaha kwa Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Raphael Tuju kwa kutumia maneno ya kumkosea heshima pamoja na jamii ya Waluo kwa jumla.
Kwenye kikao na wanahabari Jumanne katika majengo ya bunge, Bw Waluke amesema matamishi yake yalitokana na “kuteleza kwa ulimi” na kwamba “sikuwa na nia ya kumtusi Bw Tuju au jamii yake.”
“Ninaomba msamaha kwa Bw Tuju, jamii ya Waluo, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na Wakenya kwa ujumla kwa sababu matamshi niliyotoa yalimdunisha Bw Tuju. Hasa najuta kutumia neno ‘Waluo’,” amesema Waluke.
Akiongeza ujumbe wa viongozi wa makundi ya kijamii katika eneobunge lake Bw Waluke alinukuliwa akisema kuwa yeye kama kaimu naibu mwenyekiti wa Jubilee alikuwa tayari kufurusha Bw Tuju kutoka chama hicho “ili aende kwa jamii yake ya Waluo ambao husababisha fujo kila mahali.”
Sauti ya video iliyomnasa akitoa matamshi hayo na iliyosambazwa mitandaoni imeibua kero miongoni mwa Wakenya ambao wamekosoa matamshi hayo.
Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imemwamuru Bw Waluke kufika mbele yake kuhojiwa kuhusiana na matamshi hayo.