Wanamaji kuandaa gwaride Mashujaa Dei
Na ANTHONY SAISI
Kwa mara ya kwanza, jeshi la wanamaji la Kenya, litaandaa gwaride la heshima wakati wa sherehe za siku kuu ya Mashujaa zitakazoandaliwa katika bustani ya Mama Ngina, Mombasa.
Akiongea alipokagua bustani hiyo, Katibu wa wizara ya usalama wa ndani, Dkt Karanja Kibicho, alithibitisha kuwa jeshi la wanamaji litaandaa gwaride baharini na pia nchi kavu.
“Gwaride ya kitaifa itaandaliwa na jeshi la wanamaji na huenda hii ikawa ni mara ya kwanza ulimwenguni au barani Afrika kwa sababu kwa kawaida huwa inaandaliwa na jeshi la nchi kavu. Kote ulimwenguni, ni wanajeshi na ndege za kijeshi ambazo huwa zinaruka kwa kasi lakini kwa wakati huu tutatumia jeshi la wana maji,” alisema Bw Kibicho.
Alisema bustani hiyo haikukarabatiwa kwa sababu ya kuandaa sherehe hizo pekee mnamo Oktoba mbali itakuwa mahali pa watu kubarizi.
“Asilimia 95 ya kazi ya kujenga jukwaa ambalo litatoshea watu 4,000 imekamilika, kituo cha kitamaduni kinatarajiwa kukamilika katika muda wa siku 21. Umma utaendelea kutumia bustani hii baada ya sherehe,” alieleza.
Bw Kibicho ambaye alikuwa ameandamana na wenzake wa Elimu Belio Kipsang na Joe Okudo wa Utalii alisema walikagua ukarabati uliofanya katika ikulu ya Mombasa ambapo dhifa ya kitaifa itaandaliwa na kusema waliridhika.