Wanaoteremsha maski kwa kidevu washtakiwe, asema gavana
Na SAMMY WAWERU
Ni jambo la kushangaza kuona mtu akiwa na maski na kuining’iniza chini ya kidevu badala ya kuivalia ipasavyo.
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga amesema wanaofanya hivyo wanapaswa kukamatwa na kuchukuliwa hatua kisheria, kwa kile anahoji ni kujitia katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona na pia kuambukiza wengine.
Akitumia mfano wa Kaunti ya Nyeri, gavana alisema utepetevu huo unaonyesha wazi wananchi hawajali hatari inayowakodolea macho.
“Katika kaunti ya Nyeri, idadi kubwa ya wakazi ina maski ila wanaining’iniza kwenye kidevu hata wakiwa maeneo ya umma,” Bw Kahiga akasema.
“Nikielekea Embu majuzi, nilishangaa kuona baadhi ya watu Kirinyaga hawavalii maski. Matukio hayo ni taswira ya maeneo mengine nchini,” Gavana akasema.
Alisema licha ya Wizara ya Afya kuhimiza Wakenya haja ya kutilia maanani sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti kuenea kwa Covid-19, huenda jitihada hizo zikaambulia patupu endapo wananchi hawatatii.
Huku zuio la kusafiri likiwa limeondolewa, Gavana Kahiga alisema mienendo ya wananchi inachangia kuenea kwa corona kutokana na utepetevu wao.
“Itafika mahali kaunti ya Nyeri tutaamuru maafisa wa polisi kukamata na kushtaki wanaoning’niza maski kwenye kidevu, kwa kuwa wanalemaza vita dhidi ya Covid-19,” alionya.
Tangu zuio la kuingia kaunti ya Nairobi, Mombasa na Mandera kuondolewa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Julai 6, 2020, visa vya maambukizi ya corona vimeongezeka mara dufu.
Rais Kenyatta akisubiriwa kufanya kikao na magavana mnamo Ijumaa, juma hili, inahofiwa huenda serikali ikarejesha amri ya kutoingia na kutotoka nje ya kaunti zilizokuwa zimefungwa awali, kutokana na ongezeko la maambukizi.
Kufikia sasa, Kenya imeandikisha zaidi ya visa 14,000 vya maambukizi ya corona, tangu kisa cha kwanza kiripotiwe nchini mnamo Machi 13, 2020.