Habari Mseto

Wandani wa Ruto wamrai Rais Uhuru asimteme

January 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

BENSON AMADALA na SHABAN MAKOKHA

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto wamemwomba Rais Uhuru Kenyatta kutomtenga Dkt Ruto anapomaliza muhula wake wa pili kama Rais.

Viongozi hao walisema kuwa Bw Kenyatta anapaswa kurudisha mkono kwa Dkt Ruto kwa kumuunga mkono na kuhakikisha kuwa amemrithi atakapoondoka ofisini mnamo 2022.

Hiyo ndiyo ilikuwa kauli kuu iliyojitokeza kwenye mkutano wa kisiasa uliofanyika Jumamosi katika Uwanja wa Nabongo mjini Mumias.

Wakati huo huo, waliwalaumu vikali kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula kwa kutohudhuria mkutano huo, wakisema wameisaliti jamii ya Abaluhya.

Walisema kwamba walikuwa wakiwatarajia viongozi hao wawili kuhudhuria, lakini wakashangazwa na hatua yao kuwepo katika mkutano uliofanyika katika Uwanja wa Bukhungu wiki iliyopita.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale ndiye alianzisha mdahalo huo, akisema kuwa Rais Kenyatta ana deni kwa Dkt Ruto kwa kumuunga mkono kwenye chaguzi kuu za urais za 2013 na 2017.

“Dkt Ruto alimsaidia (Uhuru) kushinda urais mnamo 2013 na 2017. Yatakuwa makosa makubwa kwa Rais Kenyatta kumsahau Dkt Ruto anapomaliza vipindi vyake viwili,” akasema.

Polisi walifutilia mbali mkutano wa viongozi hao Jumamosi iliyopita, kutokana na kile walitaja kuwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, mkutano wa kuipigia debe ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) ulioongozwa na Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega uliendelea bila matatizo yoyote katika Uwanja wa Bukhungu.

Polisi pia walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya watu waliokuwa wamefika katika uwanja huo.

Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali alilazimika kujificha, akidai kuwa uhai wake ulikuwa hatarini.

Kwenye mkutano wa Jumamosi, mbunge wa Malava, Malulu Injendi alisema kuwa Rais Kenyatta hapaswi kusahau matatizo aliyokumbana nayo wakati alifikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) pamoja na Dkt Ruto nchini Uholanzi kutokana na ghasia za uchaguzi tata wa 2007/2008.

“Uamuzi wao kuhudhuria mkutano wa BBI katika Uwanja wa Bukhungu ulioyesha wazi kwamba hawafai kuwania urais,” akasema Dkt Khalwale.