Washukiwa watatu wa al-Shabaab wanaswa Thika, wahojiwa na ATPU
Na LAWRENCE ONGARO
KIKOSI cha maafisa wa usalama Kiambu kipo imara kukabiliana na uvamizi wowote unaoweza kutokea wakati wowote katika eneo hilo.
Kamanda mkuu wa Polisi katika kaunti hiyo, Bw Ali Nuno, alisema Jumanne jioni kwamba ikizingatiwa uvamizi ambao ulishuhudiwa maeneo ya Lamu na sehemu za Mandera na Garissa hivi majuzi, kikosi cha usalama katika eneo hili kipo chonjo kukabiliana na tishio lolote lile.
Alisema ili kuthibitisha usemi wake, tayari maafisa wa polisi katika eneo hilo la Kiambu wamewanasa washukiwa watatu wa al-Shabaab, ambao tayari wanaendelea kuhojiwa katika kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU).
“Wawili kati ya washukiwa hao walinaswa wiki mbili zilizopita katika barabara kuu ya Garissa-Nairobi wakiwa wameabiri basi kuelekea jijini Nairobi. Mwingine wa watatu alinaswa katika mtaa wa Makongeni, Thika wiki mbili zilizopita,” alisema Bw Nuno.
Alieleza kuwa maafisa wa usalama katika kizuizi cha kuingia mjini Thika katika barabara kuu ya Garissa-Nairobi wanachunguza kwa kina vitambulisho vya wasafiri wote wanaoingia kutoka Kaskazini Mashariki mwa nchi.
Alisema maafisa wa polisi ambao wanajihusisha na uhalifu watachukuliwa hatua ya kisheria.
Aliongeza kuwa kila afisa wa polisi ni sharti afuate sheria.
Mnamo Jumatatu, afisa wa polisi alifikishwa katika mahakama ya Thika kwa tuhuma ya kushirikiana na mwanafunzi wa chuo kikuu na kuiba pombe katoni kadhaa kutoka kwa kiwanda kimoja cha mvinyo na pombe mjini Thika.
Ushauri
Alisema polisi yeyote atakayepatikana na makosa ya uhalifu ataubeba msalaba wake mwenyewe huku akiwashauri watekeleze wajibu wao kwa njia inayofaa.
Kamishna wa Kaunti ya Kiambu, Bw Wilson Wanyanga alisema hali ya usalama inashughulikiwa vilivyo ambapo tayari amewahakikishia wakazi wa Kiambu wasiwe na wasiwasi bali waendelee na mambo na shughuli zao kama kawaida.
“Tunajua al-Shabaab sasa wanavizia nchi yetu ya Kenya. Pia upo uhasama baina ya Amerika na Iran. Kwa hivyo usalama unatiliwa maanani ambapo walinda usalama watapiga doria muda wa saa 24 bila kupumzika,” alisema Bw Wanyanga.
Aliyasema hayo Jumanne mjini Thika alipokutana na maafisa wakuu wote wa Kaunti ya Kiambu, pamoja na machifu na manaibu wao. Maafisa hao walitoka Juja, Gatundu Kusini na Kaskazini, Thika Mashariki na Magharibi, na Ruiru.
Alitoa mwito kwa wananchi popote walipo kushirikiana na walinda usalama na kuripoti jambo lolote lisilo la kawaida.