Habari Mseto

Wauguzi Kisumu wasisitiza hawarudi kazini hadi walipwe mshahara wa Januari

February 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BRENDA AWUOR

WAGONJWA katika hospitali zilizopo Kaunti ya Kisumu, watalazimika kupokea matibabu kutoka hospitali za wamiliki binafsi baada ya wauguzi kusisitiza hawarudi kazini hadi watakapopokea mshahara wao wa mwezi wa Januari.

Baada ya wafanyakazi wa Kaunti ya Kisumu kupokea ujumbe wa kupata msharaha wao kupitia hundi na kusubiri hadi Februari 10, walilazimika kutembelea ofisi ya gavana Prof Peter Anyang’ Nyong’o, huku wakimtaka mwenyewe kuwaeleza sababu ya wao kutolipwa jinsi walivyoagana.

Wafanyakazi hao waliowakilishwa na mwenyekiti wa wafanyikazi, Bw Edward Kojiema, Katibu wa idara ya wafanyakazi maabarani, Bw Hillary Awili na katibu wa wafanyakazi Bw Craus Okumu, wamesisitiza wataendelea kuandaa gwaride la kuitisha mshahara – salary parade – eneo la ofisi ya gavana na kutorudi kazini hadi watakapopokea mshahara wao wa Januari.

Msemaji wa gavana wa Kisumu, Bw Aloyce Ager, akiongea na wanahabari, amehimiza wafanyakazi hao warudi kazini kwa kuwa “kuanzia Jumatano wiki ijayo watapokea mshahara”.

Bw Ager ameeleza kuwa pesa tayari zipo kwenye benki na kufikia Jumatano hundi zote zitakuwa tayari kuchukuliwa na wafanyakazi.

Ameonya wafanyikazi dhidi ya kuandaa mgomo kila mara wanapokumbwa na tatizo lolote.

Kaunti ina wafanyakazi zaidi ya 4,000 na kila mmoja licha ya kutopokea mshahara wa Januari ni muhimu waendelee kufanya kazi huku wakiwa na imani ya kupokea mshahara wao wiki ijayo, amesema.

”Kila mfanyakazi wa kaunti, mimi mwenyewe nikiwemo, hatujapokea mshahara wa Januari ila tupo kazini na ndiposa nawasihi wauguzi warejee hospitalini wakiwa na matumaini ya kupokea mshahara wao Jumatano,” amesema Bw Ager.