• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Wazazi wa Kyanguli hatimaye wafidiwa Sh53m

Wazazi wa Kyanguli hatimaye wafidiwa Sh53m

Na LILLIAN MUTAVI

WAZAZI ambao wanao waliangamia kwenye mkasa wa moto katika Shule ya Wavulana ya Kyanguli, Kaunti ya Machakos jana walipata fidia ya Sh53 milioni baada ya kusubiri kwa muda wa miaka 18.

Kisa hicho cha maangamizi kilitokea mnamo Machi 24, 2001 wakati bweni la shule hiyo lilipoteketea na kusababisha mauti ya wanafunzi 67.

Mwenyekiti wa shule hiyo Hillary Kitata alisema kwamba karibu wazazi wote wamepokea hundi zao kutoka kwa serikali isipokuwa wachache ambao bado hawajawasilisha stakabadhi za kuonyesha kwamba walikuwa wazazi wa wanafunzi walioangamia.

“Jumla ya Sh53 milioni zimelipwa kwa wazazi 63 na kuna masalio ya Sh7 milioni ambayo bado hayajalipwa. Tuna matumaini waliosalia watalipwa kabla ya mwaka kukamilika,” akasema Bw Kitata.

Wakili Kioko Kilukumi ambaye aliwakilisha familia za wanafunzi hao, alisema kila mzazi alipokezwa Sh786,000 akiongeza kuwa wazazi hao wataanzisha miradi nyumbani kwao kama njia ya kuwaenzi na kuwakumbuka wanao.

“Kila mzazi atawekeza kwenye miradi ya kumkumbuka mwanawe. Wengine watawekeza kwenye kilimo, kuchimba visima na kufadhili elimu ya watoto wao,” akasema Bw Kilukumi. Mzazi Stella Kiluu, mamaye marehemu Kitata Kiluu alishukuru serikali kwa kutimiza ahadi kwa kulipa fedha hizo ambazo angalau zitawapunguzia huzuni na uchungu wa kuwapoteza watoto wao.

Marehemu BW Kitata alikuwa kifungua mimba kwenye familia hiyo na mamake sasa anasema atatumia fedha hizo kuanzisha mradi wa kumuenzi japo hakuufichua utakuwa upi.

Bi Kiluu aliongeza kuwa kama wazazi wa marehemu, wataendelea kuandaa mikutano na kushauriana kuhusu masuala mbalimbali .

You can share this post!

Deni la mabilioni lamwandama Biwott kaburini

Gaidi aliyeuawa Kwale alihusika katika uvamizi Dusit...

adminleo