Habari Mseto

Wazazi wasaka waganga kutambua wanafunzi wanaochoma shule

May 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

WAZAZI wa shule ya Upili ya wavulana ya Lamu Bujra sasa wanautaka usimamizi wa shule hiyo kutafuta huduma za mpiga ramli na mtu wa kuapiza ili kuwatafuta na kuwatambua wanafunzi wanaojihusisha na visa vya kuchoma mabweni shuleni humo kama ilivyoshuhudiwa katika siku za hivi karibuni.

Mnamo Alhamisi wiki iliyopita, shule hiyo ilifungwa kwa muda usiojulikana baada ya moto kuzuka mara tatu na kuchoma mabweni katika kipindi cha juma moja pekee.

Mali ya mamilioni ya fedha, ikiwemo magodoro na vitanda zaidi ya 100, masanduku na nguo za wanafunzi viliunguzwa kwenye mikasa hiyo ya moto.

Wakizungumza na wanahabari shuleni humo Jumatatu aidha, baadhi ya wazazi walisema itakuwa vigumu kwa utawala wa shule hiyo kuwagundua wahusika wakuu wa visa vya moto.

Wakiongozwa na mzee Mohamed Shee Ali,60, wazazi waliushauri usimamizi wa shule hiyo kugeukia huduma za waganga, wapiga ramli na watu wa kuapiza ili kuwatambua wahusika na kuwaadhibu.

Bw Shee alisema wanafunzi wa shule hiyo wamedhihirisha utundu na kukosa nidhamu.

Alisema ni vigumu kwa wanafunzi hao kujitokeza na kuwataja kwa hiari wenzao wanaohusika na uchomaji wa mabweni na uharibifu wa mali ambao umekuwa ukiendelea shuleni humo.

Alisema anaamini iwapo mpiga ramli na mtu wa kuapiza ataletwa shuleni humo, maovu yataweza kugunduliwa kiurahisi kuliko kutiumia ngiuvu za polisi.

“Hawa wanafunzi wamedhihirisha utundu usio na kifani. Cha msingi ni usimamizi wa shule ufikirie kuleta waganga, wapia ramli na waapizaji hapa ili kuwasaka na kuwatambua hao wanafunzi wakaidi ili waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.

Wakifanya hivyo ninaamini niodhamu itarejea hapa shuleni Bujra. Kutumia polisi ni kupoteza wakati kwani wanafunzi hawa ni watundu na kamwe hawawezi kutajana licha ya kwamba wanawajua wahusika wa mikasa ya moto,” akasema Bw Shee.

Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Bi Mariam Mohamed, aliyesema kuna haja ya mbinu za kawaida zinazotumiwa kuwasaka washukiwa wa visa vya moto shuleni kubadilishwa kwanio hazijakuwa zikifanya kazi ipasavyo.

“Wanafunzi wa hapa shuleni Bujra wamezoea kwamba punde mikasa kama hiyo inapotokea, polisi wanaitwa kuwakamata baadhi yao na kisha kuachiliwa na kusahauliwa. Mara hii tuko tayari kwa waganga na wapiga ramli waitwe hapa shuleni ili kuwafichua hao wanafunzi watundu,” akasema Bi Mohamed.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wazazi (PTA) shuleni humo, Bw Feiswal Abdalla, aliwataka wazazi kuwa watulivu wakati bodi ya shule inapoendelea na uchunguzi kuhusiana na mikasa ya moto shuleni humo.

“Tuliafikia kuifunga shule ili kupisha uchunguzi kufanywa. Wazazi wawe watulivu huku usimamizi wa shule ukiendeleza harakati za kutafuta chanzo cha mikasa ya moto na pia wahusika wa uharibifu huo. Wanafunzi na wazazi watatangaziwa ni lini shule hiyo itafunguliwa punde uchunguzi utakapokamilika,” akasema Bw Abdalla.