Habari Mseto

Wito kwa jamii ya Wakamba iitishe matangi ya maji kama mahari

July 9th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PIUS MAUNDU

WAZIRI wa Maji katika Kaunti ya Makueni, Bw Robert Kisyula, ameomba jamii ya Wakamba itafakari upya utamaduni wake kuhusu mahari ili kukabiliana na uhaba wa maji unaokumba eneo hilo mara kwa mara.

Bw Kisyula alisema wazazi wanafaa wakome kuitisha mifugo kama mahari na badala yake wawe wakiitisha matangi ya maji ili kuhifadhi maji ya mvua.

“Wale wanaooza mabinti zao wanaafaa waitishe angalau matangi mawili ya lita 10,000 badala ya mbuzi na zawadi zingine,” akasema alipozindua mradi wa maji wa Masue.

Mradi huo wa Sh5.6 milioni, ambao utakuwa ukihifadhi maji ya mvua katika kijiji cha Masue, unatekelezwa kwa ushirikiano wa serikali ya kaunti na Shirika la Maendeleo la Anglikana tawi la Mashariki.

Eneo la Ukambani hutegemea uhifadhi wa maji ya mvua kwa sababu ya uhaba uliopo na kulingana na Bw Kisyula, kuitisha matangi kama mahari kutasaidia kuhakikisha familia nyingi zimehifadhi maji ya kutosha kutaimarishwa ikiwa wakazi wataukumbatia kibinafsi.

Ili kuimarisha uhifadhi wa maji zaidi, serikali ya kaunti hiyo huhitaji wanaojenga nyumba mjini waeleze kwanza jinsi wanavyopanga kuhifadhi maji ya mvua kabla waruhusiwe kujenga.

Pendekezo la Bw Kisyula limeibua mijadala hasa katika mitandao ya kijamii ambapo kuna wanaolisifu na kusema litasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa maji Ukambani.

“Tayari tumekumbatia pendekezo la Bw Kisyula nyumbani kwangu. Hakuna vile nitakubali kuchukua mbuzi kama mahari ya binti yangu.

Anayetaka kumwoa lazima ajiandae kununua matangi makubwa ili kumwondolea mamake matatizo ya kusukuma maji kwa punda,” akasema Bw Benjamin Kitua, ambaye ni mfanyabiashara anayefanya kazi Nairobi.