Amkeni! Majirani Tanzania walemewa kulipa mikopo ya simu
BAADHI ya Watanzania sasa wanalemewa kulipa mikopo yao waliyopokea kwa njia ya simu baada ya mchakato wa utoajia mikopo hiyo kuonekana rahisi kupata na kulipa kupitia matangazo ya kibiashara.
Walioathiriwa walishawishiwa kuchukua pesa hizo za haraka ambazo zimekuwa ngumu kulipa huku riba ikizidi kupanda.
Wengi wanaotaabika ni vijana wadogo na watu wenye mapato ya chini baada ya kuvutiwa na matangazo ya kibiashara kwenye vyombo vya habari nchini humo.
Wanaokopa pesa hizi aghalabu hawajui hatari zinazowakodolea macho katika sekta ya biashara ambayo haijadhibitiwa kikamilifu.
Rashid Mwenda ni mmoja wa Watanzania ambao waliathiriwa vibaya na hatua ya kuchukua mikopo ya haraka kwa njia ya mitandao.
Anasema uvumi ulisambaa kwa mapana kuwa alichukua mkopo wa simu, taarifa ambazo ziliishia kufika kwa mwajiri wake ambaye alimfuta kazi.
“Tangu nilipochukua mkopo tatizo lilianza na uvumi ukaenea na baadhi ya watu wakaenda kwa mwajiri wangu ambaye alinifuta kazi,” anasimulia Rashid bila kueleza zaidi.
“Ilikuwa ni miaka mitano iliyopita lakini hadi sasa maisha yangu hayajarejelea hali ya kawaida. Maisha yangu yameharibika na mapato yangu yanaendelea kupungua kwa sababu ya riba hii.”
Idadi kubwa ya watu waliokumbwa na hali hii ni walio na mapato madogo.
Vijana wachanga wanaopenda mitandao ya kijamii ndio waathiriwa wakubwa zaidi huku kampuni za kutoa mikopo zikiongezeka na kutoa mikopo kwa watu ambao hata hawastahiki kupewa pesa hizi.
Wanafunzi pia wameathiriwa kwa kupokea mikopo hii ya simu huku wengine wakifurahia huduma hizi za pesa mitaani kwa kuacha vyeti vyao vya shule kama dhamana.
“Kuna mashirika yanayotoa mikopo hii kwa wananchi kinyume cha sheria,” mzazi mmoja alifichua.” Nyingi ya kampuni hizi hazina hata leseni.”
Taabu wanazopitia wananchi sasa zimevutia mamlaka husika nchini Tanzania ambayo imeingilia kati na kufuta mikopo yote kwa njia ya mitandao.
Eric Makundi mfanyakazi wa shirika la fedha anaeleza: “Tunatuhumiwa kuwa kampuni za kukopesha zimekuwa nyingi na tunatoa pesa kwa watu ambao hawana sifa hata ya kukopesheka almuradi watu wana simu na kadi ya mawasiliano.”
Baadhi ya mashirika yanayotoa mikopo yamefungwa kwa sababu ya kuendeleza oparesheni bila kuwa na leseni.
Benki kuu ya Tanzania imechukua hatua kuthibiti mashirika haya madogo ya fedha kufuatia utoaji wa mikopo kinyume cha sheria.
“Tumechukua hatua zingine kwa ushirikiano na vyombo vya usalama. Katika mikoa ya Songwe, Dodoma, Kagera, Mwanza na Mtwara, tumekamata wale ambao wanatoa mikopo bila leseni na sasa hivi wanaendelea kujibu mashtaka mahakamani,” alisema afisa wa Benki Kuu ya Tanzania.
Watanzania wanatakiwa kuwa makini na kutathmini masharti ya utoaji mikopo kabla ya kuipokea kwa njia ya mitandao.