2019 utakuwa mwaka wa njaa – Ripoti
KEVIN J KELLEY na BARNABAS BII
KENYA huenda ikakabiliwa na baa la njaa mwaka 2019 kutokana na mavuno duni, haya ni kwa mujibu wa utabiri wa Shirika la Kutafiti Uwepo wa Chakula katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki linalofadhiliwa na Amerika.
Shirika hilo limetoa tahadhari kuwa mavuno yatapungua kwa asilimia 30 katika miezi michache ya mwanzoni mwa 2019 hivyo kusababisha nchi kutumbukia katika baa la njaa.
“Uzalishaji wa chakula nchini Kenya na Somalia utapungua kwa asilimia 30 chini ya kiwango cha wastani. Malisho ya mifugo na maji pia huenda yakawa adimu,” ikasema taarifa ya shirika hilo linalofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Amerika (Usaid).
“Iwapo utabiri huo utatimia, kutakuwa na uhaba wa chakula nchini Kenya na Somalia. Mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yanafaa kujiandaa kukabiliana na baa la chakula mwaka wote wa 2019,” likaongeza.
Makali ya baa la njaa yatashuhudiwa zaidi katika Kaunti za Makueni, Kitui na Taita Taveta.
Shirika hilo lilisema kuwa wafugaji wanaendelea kuhamisha mifugo wao kutafuta malisho na maji nchini Somalia na hali sawa na hiyo huenda ikaanza kushuhudiwa humu nchini hivi karibuni.
“Kuanzia Januari, kutakuwa na uhaba wa maji, kupungua kwa maziwa kati ya changamoto nyinginezo zinazosababishwa na ukame,” likaonya shirika hilo.
Shirika hilo, hata hivyo, linasema kuwa mavuno mengi yaliyopatikana mwaka huu yatasaidia pakubwa katika kukabiliana na baa la njaa 2019.
“Idadi ya Wakenya watakaokabiliwa na baa la njaa katika miezi ya mwanzo ya 2019 itakuwa ya juu zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali,” linasema shirika hilo.
Wakati huo huo, mamia ya familia ambazo mazao yao yaliharibiwa na nzige katika Kaunti ya Turkana, zinahitaji chakula cha msaada kwa dharura.
Familia hizo kutoka eneo la Kibish na eneobunge la Turkana Kaskazini jana waliitaka serikali pamoja na mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu kuwapa chakula baada ya mashamba yao zaidi ya ekari 10,000 kuharibiwa na nzige.
“Nzige hao wametusababishia njaa licha ya juhudi za serikali ya kaunti kukabiliana nao kwa kunyunyuzia dawa ya kuua wadudu,” akasema mbunge wa Turkana Kaskazini Christopher Nakuleau.
Kulingana na Bw Nakuleau, zaidi ya watu 250,000 kutoka eneo hilo wanahitaji msaada wa chakula kwa haraka.
“Serikali ya kitaifa na mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu na wahisani wengineo hawana budi kuingilia kati na kuwakinga waathiriwa hao wa nzige dhidi ya njaa,” akasema Bw Nakuleau.
Alisema baadhi ya wafugaji wamehamia katika mipaka ya Kenya na Sudan Kusini na Ethiopia kutafuta malisho na maji baada ya kutokea ukame katika eneo hilo.