BAJETI: Raila ala minofu Ruto akipiga miayo
Na PAUL WAFULA
SERIKALI haijakoma kumkata miguu Naibu Rais William Ruto, wakati huu ikipunguza bajeti yake ya mwaka ujao wa kifedha kwa karibu Sh1 bilioni.
Bajeti hiyo ya ofisi ya Dkt Ruto imepunguzwa kwa jumla ya Sh988 milioni huku ya ofisi ya Rais Uhuru Kenyatta ikipanda kutoka Sh11.4 bilioni hadi Sh36.6 bilioni.
Kwa upande mwingine, Kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa mara ya kwanza kama Kiongozi Rasmi wa Upinzani amepewa mamilioni ya pesa kwenye bajeti kuu itakayosomwa leo Alhamisi, baada ya ofisi yake kutengewa Sh71.9 milioni.
Lakini licha ya kutengewa pesa hizo kama Kiongozi wa Upinzani, Bw Odinga ‘hayuko katika upinzani’ bali ni mtetezi wa Serikali.
Bw Odinga ambaye anatafuna matunda ya handisheki kati yake na Rais Kenyatta pia ametengewa Sh26 milioni za kununua magari, Sh20 milioni za bima na Sh10 milioni za fanicha.
Awali Serikali ya Jubilee ilikuwa ikikataa kuipatia ofisi ya Bw Odinga pesa kama Kiongozi wa Upinzani, ikidai kwanza astaafu kutoka siasa, lakini hitaji hilo sasa halipo baada yake kukubali kuacha kuwa mkosoaji wa Serikali.
Kwa upande wake, Dkt Ruto atakuwa na uhaba wa pesa baada ya bajeti ya ofisi yake kupunguzwa hadi Sh1.4 bilioni kutoka Sh2.4 ilizopewa mwaka huu wa kifedha unaokamilika.
Pesa za kusafiri za Naibu Rais nazo zimepunguzwa kutoka Sh193 milioni hadi Sh96 milioni, katika juhudi za kuzima ziara zake nyingi za kujipigia debe kwa ajili ya uchaguzi wa 2022, safari ambazo zilifanya kundi lake libandikwe jina “Tangatanga”.
Katika kuhakikisha Dkt Ruto amelemazwa zaidi, Waziri wa Fedha Ukur Yattani amekata bajeti yake ya kusafiri nje ya nchi kutoka Sh 89 milioni hadi Sh33 milioni.
Bajeti ya kuburudisha wageni wa Naibu Rais nayo imepunguzwa kutoka Sh197 milioni hadi Sh87 milioni, ya petroli ikashuka kutoka Sh28 milioni hadi Sh 14 milioni huku ya shughuli za kila siku za ofisi ikishuka kwa asilimia 66 kutoka Sh 307 milioni hadi Sh103 milioni.
Ingawa Serikali imesema inapunguza bajeti yake ya matumizi ya kila siku, ukweli kuwa ofisi ya Dkt Ruto ndiyo imepunguziwa pesa zaidi kuliko zingine zote inaonyesha kuendelezwa kwa harakati za kumnyoa mabawa zaidi.
Kwenye bajeti hiyo itakayosomwa na Bw Yattani, serikali imeacha kutengea pesa ofisi ya marehemu rais wa pili Daniel Moi, huku ofisi ya rais wa tatu Mwai Kibaki ikipunguziwa bajeti kutoka Sh133 milioni hadi Sh113 milioni.
Pigo hilo la kifedha kwa Dkt Ruto ndilo la majuzi kabisa baada ya ushawishi wake katika Seneti, Bunge la Taifa na chama cha Jubilee kufutwa.
Hii ni baada ya Rais Kenyatta kuongoza kampeni ya kuwang’oa madarakani viongozi waliokuwa wakiegemea upande wa naibu wake, hali ambayo imeyeyusha usemi aliokuwa nao serikalini.
Rais Kenyatta pia anatarajiwa kufanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri wakati wowote kuanzia leo, katika juhudi za kupunguza zaidi uwezo wa Dkt Ruto kisiasa.
Duru zinaeleza kuwa mawaziri wawili kutoka Rift Valley watalishwa sakafu kwenye mabadiliko hayo. Pia kuna waziri mmoja kutoka eneo la Mlima Kenya ambaye pia anatarajiwa kutumwa nyumbani.
Rais Kenyatta ametetea harakati za kumnyoa naibu wake, akisema anataka kuteua watu ambao watamsaidia kutimizia ahadi zake kwa Wakenya.
Wakereketwa wa Rais Kenyatta wanamlaumu Dkt Ruto wakisema anahujumu ajenda ya Rais kwa kuanza kampeni za mapema za kuwania urais hapo 2022.