Chiloba sasa amshtaki Chebukati
Na CHARLES WASONGA
AFISA Mkuu Mtendaji wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Alhamisi amewasilisha kesi mahakamani kupinga uamuzi wa tume hiyo kumpa likizo ya lazima.
Uamuzi huo ulitangazwa wiki iliyopita na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati baada ya kukutana na makamishna wenzake kujadili ripoti ya ukaguzi wa matumizi ya fedha katika IEBC wakati wa uchaguzi mkuu mwaka.
Kwenye stakabadhi zilizowasilishwa katika Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Leba Alhamisi na wakili wake Andrew Wandabwa, Bw Chiloba anataka mahakama hiyo kubatilisha hatua hiyo.
Vile vile, anataka Bw Chebukati analazimishwe kufichua na kufafanua makosa katika ununuzi wa bidhaa anayotuhumiwa kutenda katika kipindi hicho cha uchaguzi, yaliyotajwa kama mojawapo ya sababu ya kufurushwa kwake.
Vile vile, Chiloba anasema uamuzi wa kumwagiza aende nyumbani ulifikiwa bila kufuata kanuni na ulikiuka haki yake ya kupewa nafasi ya kujitetea.
“Hatua hii ni kinyume cha sheria za IEBC ambazo hazimruhusu mwenyekiti kuingilia majukumu ya sekritariati,” akasema.
IEBC ilimtuma Chiloba likizo ya miezi mitatu kutoa nafasi ya uchunguzi kufanywa kuhusiana hitilafu zilizobainika katika idara ya ununuzi bidhaa na huduma kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.
Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano ulioongozwa na Chebukati na kuhudhuria na naibu wake Consolata Bocha Maina na makamishna, Boya Molu, Profesa Abdi Guliye na Dkt Paul Kurgat.
Hata hivyo, Bi Maina na Dkt Kurgat walipinga uamuzi huo wa kumsimamisha kazi Bw Chiloba wakisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumhusisha afisa huyo na hitilafu hizo.
Hitilafu hizo hazikutajwa katika barua ambayo Bw Chebukati alimtumia Chiloba Ijumaa wiki iliyopita kumwagiza kwenda likizo ya miezi mitatu.