Habari

Corona yaongeza upweke wa Ruto

April 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MASHARTI makali yaliyotangazwa na Wizara ya Afya kudhibiti kuenea kwa virusi hatari vya corona yanaendelea kumzidishia upweke Naibu Rais William Ruto ambaye masaibu yake ya kisiasa yanaendelea kuongezeka kila uchao.

Dkt Ruto amekuwa akijikakamua pakubwa kuonyesha angali ngangari licha ya misukosuko inayokumba chama cha Jubilee, ishara kuwa ametengwa katika shughuli muhimu za serikali kuu.

Na sasa, janga la corona limeonekana kuvuruga mipango yake kisiasa.

Mnamo wikendi, hali halisi ya upweke wake ilidhihirika kwa namna ambayo aliendeleza ibada ya Jumapili nyumbani kwake.

Kabla ya ibada za makanisa kusimamishwa nchini Machi kutokana na tishio la janga la corona, Dkt Ruto alikuwa kipenzi cha viongozi wengi wa makanisa, wakipigania kumwalika kwenye michango yao.

Wanasiasa wengi, hasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ walikuwa wakiandamana naye kwenye makanisa hayo, huku wakitumia majukwaa waliyopewa kuujibu Upinzani na yeyote waliyehisi “anamwingilia” Dkt Ruto.

Lakini Jumapili, ilibainika siku hizi analazimika kuandaa ibada na familia yake pekee kwenye chumba maalum cha maombi kilicho katika makao yake rasmi mtaa wa Karen, jijini Nairobi.

Kwenye picha alizoweka kwenye ukurasa wake wa Facebook, Dkt Ruto alikuwa na mkewe, Bi Rachael Ruto na watoto wao sita pekee huku chumba kizima kikiwa na viti tupu. Yeye na mkewe ndio walioongoza ibada.

Hili ni kinyume na ibada alizohudhuria, alikoalikwa na kupokelewa kwa shangwe na maelfu ya watu.

Na kama ishara ya kujiliwaza kutokana na hali inayomkabili, alinukuu kitabu cha Zaburi 27: 1-4 kwenye Biblia: “…wakati mahasidi wangu wanaungana kunimaliza, wao ndio watakaoangamia. Ingawa jeshi linaweza kuungana dhidi yangu, sitaogopa. Hata ikiwa vita vitaelekezwa kwangu, nitaendelea kuamini.”

Katika chama cha Jubilee, Naibu Rais angali anapigwa vita huku chama kiking’ang’aniwa kati ya upande wake na ule unaoegemea Rais Uhuru Kenyatta.

Dkt Ruto anapotikiswa na mawimbi ya kisiasa chamani ambapo anastahili kuwa na mamlaka makubwa kama naibu kiongozi, wandani wake wengi wamebaki kimya ikilinganishwa na awali.

Wengi wao wanasema wameamua kuendesha utetezi wao “kichinichini” kama vile kupitia mitandao ya kijamii, bila kutoa matamshi yoyote makali ilivyokuwa awali.

Wanadai kwamba si lazima waonekane wakimtetea hadharani, wakisisitiza kuwa “kuna njia nyingi.”

Miongoni mwa wanasiasa walioenda chini ya maji ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri, wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Ndindi Nyoro (Kiharu), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Rigathi Gachagua (Mathira), Seneta Aaron Cheruiyot (Kericho) kati ya wengine.

“Vita vyetu vya kuikomboa Kenya bado vinaendelea. Hatutatikisika,” alisema Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro ambaye ni mmoja wa watetezi wakuu wa Dkt Ruto.

Kanuni za kuzuia watu kukongamana pia zimezima ziara nyingi za makundi ya kijamii na kidini ambazo zilikuwa zikifanywa nyumbani kwake Karen jijini Nairobi na Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu mara kwa mara.

Katika shughuli za kiserikali, Naibu Rais ameonekana kutengwa katika mikakati ya kupambana na janga la corona hata ingawa anasisitiza wanawasiliana kila mara na Rais.

Rais hukutana na viongozi mbalimbali kupanga mikakati ya kupambana na corona wakiwemo magavana, lakini ni nadra sana Dkt Ruto kuandamana naye.

Hali hii imefanya juhudi za ‘Tangatanga’ kueneza ajenda zao kwa ukakamavu kama zamani, wakati ambapo kuna madai kwamba Jubilee inapanga kuunda muungano na vyama vya ODM na Kanu kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao.