Habari

Ethekon- IEBC imesajili wapiga kura wapya 90,020, Nairobi ikiongoza

Na CHARLES WASONGA November 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa imesajili jumla ya wapiga kura wapya 90,020 kufikia Oktoba 31, 2025.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Novemba 2, 2025, mwenyekiti wa tume hiyoo, Erustus Ethekon, alisema idadi hiyo inaonyesha kuwa asasi hiyo imepiga hatua katika zoezi hilo lililoanza kote nchini mnamo Septemba 29, isipokuwa katika maeneo 24 ambako chaguzi ndogo zitaendeshwa Novemba 27.

Kulingana na mwenyekiti huyo, kaunti ya Nairobi inaongoza kwa kuwasajili wapiga kura wapya 16,512, ikifuatwa na Kiambu iliyoandikisha wapiga kura 9,917 huku Machakos ikishikilia nambari tatu kwa kuandikisha watu 4, 026.

Kaunti zingine ambazo zimesajili zaidi ya wapiga kura wapya 3,000 ni; Mombasa (3,967), Kitui (3,552, Murang’a (3,330), Nakuru (3,265) huku Meru ikiandikisha wapiga kura 3, 128.

Kwa upande mwingine, kauti za Tana River, Isiolo, Samburu, Nyamira, Marsabit na Elgeyo Marakwet zimeandisha idadi ya wapiga kura wapya wasiodizi 400, tangu zoezi hilo lilipoanza.

Kaunti ya Tana River imesajili wapiga kura 130 pekee na hivyo kuorodhewa kama iliyoandikisha watu wachache mnamo.

Hata hivyo, Bw Ethekon alielezea kufurahishwa kwake na idadi jumla ya Wakenya ambao wamejisajili akisema inaashiria kuwa tume hiyo inapiga hatua nzuri katika zoezi hilo.

“Hatua hii inaakisi kujitolea kwa IEBC kutimiza wajibu wake kulingana na kipengele cha 88 (4) cha Katiba wa kufanikisha usajili wa wapiga kura karika maeneo bunge yote 290,” akaeleza Bw Ethekon.

“Aidha, raia wanajitokeza kubadilisha vituo vyao vya kupigia kura na maelezo yao kwenye sajili ya wapiga kura ishara kwamba wanatambua umuhimu wa shughuli hii itakayowawezesha kuwachagua viongozi wanaowataka,” akaongeza.

Vile vile, IEBC ilitoa wito kwa wadau, kama vile vyama vya kisiasa, mashirika ya kijamii, mashirika ya kidini na vyombo vya habari kuendelea kuwahimiza raia wajitokeze kujisajili, “kuthibitisha maelezo yao na kuhamia vituo vya kupigia kura wanavyovitaka.”