Habari

Gachagua asusia ibada ya wafu ya Raila

Na BENSON MATHEKA October 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUKOSEKANA kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika ibada ya kitaifa ya wafu ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Amolo Odinga kumeibua maswali miongoni mwa Wakenya, huku wengi wakijiuliza sababu ya kutofika kwake kwenye hafla hiyo muhimu ya kitaifa iliyofanyika Ijumaa, jana katika Uwanja wa Nyayo.

Hii ni kwa kuwa viongozi wengine wa upinzani kama vile Kalonzo Musyoka, Fred Matiang’i, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Justin Muturi, waliungana na viongozi wa serikali kuonyesha mshikamano wa kitaifa na kumuenzi Raila kama kiongozi aliyegusa maisha ya Wakenya wengi.

Wengi walitarajia kwamba Gachagua naye angejitokeza, hasa ikizingatiwa kuwa aliyekuwa mpinzani wake mkubwa kisiasa, Rais William Ruto, alihudhuria na kutoa heshima zake za mwisho.

Uhusiano kati ya Raila na Gachagua ulikuwa na changamoto nyingi, hasa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2022. Gachagua, akiwa mgombea mwenza wa Ruto kupitia muungano wa Kenya Kwanza, alimshambulia Raila vikali, akimtaja kama “mradi wa serikali” wa Rais wa wakati huo, Uhuru Kenyatta.

Raila pia aliunga kutimuliwa kwa Gachagua kupitia mchakato wa Bunge mwaka jana. Bw Gachagua huwa anaepuka kuketi jukwaa moja na Rais Ruto tangu walipotofautiana kisiasa hadi akatimuliwa serikalini.