Habari za Kaunti

Aladwa sasa alenga uenyekiti wa ODM Nairobi baada ya kutamba Makadara

Na KEVIN CHERUIYOT April 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Makadara George Aladwa  Jumatano aliwasifu wanachama wa ODM kwa kudumisha amani walipokuwa wakishiriki uchaguzi wa mashinani wa chama hicho katika Kaunti ya Nairobi.

Kura ya mashinani ya ODM Jumatano ilifanyika kwenye maeneobunge ya Makadara, Kibra na Westlands ambapo wanachama walishiriki shughuli hiyo kwa njia ya amani.

Mamia ya wafuasi wa ODM kutoka Makadara walijibwaga barabarani kushangilia na kusherehekea Bw Aladwa kudumisha wadhifa wake wa uenyekiti bila kupingwa. Hatua hiyo sasa inamweka mwandani huyo wa Kinara wa ODM Raila Odinga, pazuri kutetea wadhifa wake kama mwenyekiti wa chama katika Kaunti ya Nairobi.

“Nataka niwashukuru wafuasi wangu kwa kunichagua bila kupingwa na kudumisha amani tangu Jumatatu wakati kura zimekuwa zikiendelea kwenye wadi mbalimbali Nairobi,” akasema Bw Aladwa anayehudumu muhula wake wa  pili bungeni kwa tikiti ya ODM.

“Nataka niweke wazi kuwa nitakuwa nikitetea wadhifa wangu kama mwenyekiti wa ODM Nairobi. Niko tayari kumenyana na wapinzani wangu na nitakubali matokeo wakati kura hiyo itafanyika,” akaongeza.

Alikashifu ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa baadhi ya maeneo ya nchi wakati wa uchaguzi huo wa kiwango cha wadi, akisema zinasawiri chama kama kinachovumilia fujo.

“Hakuna haja ya kupigana kwa sababu viti ni vingi na pia wanaoshindwa wakubali matokeo. Tusipigane na kusawiri chama vibaya ilhali tunastahili kukikuza,” akasema.

Kati ya visa vya ghasia ambavyo vimeripotiwa ni mnamo Jumatatu ambapo watu wawili walikatwa mikono katika uchaguzi wa ODM eneobunge la Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay.