Habari za Kaunti

Himizo serikali ikwamue miradi ya maji iliyokwama maeneo kame

Na STANLEY NGOTHO November 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAMATI ya Bunge la Kitaifa ya Ustawi wa Kimaeneo imeomba serikali itoe fedha za kufadhili miradi muhimu ambayo imekwama na kuathiri vibaya maisha ya wananchi wa kawaida.

Wakizungumza walipokuwa wakikagua miradi kadhaa Kaunti ya Kajiado, wanachama wa kamati hiyo walisema kuchelewa kwa fedha za kutosha kumesababisha utepetevu miongoni mwa wakandarasi.

“Serikali imejitolea kutenga fedha kwa ajili ya ustawishaji wa kikanda. Kamati hii itahakikisha hazina ya maendeleo ya kimaeneo haiondolewi na badala yake iimarishwe,” alisema Mwanachama Peter Nabulindo, Mbunge wa Matungu mnamo Jumamosi.

Wabunge hao walitambua kuwa upatikanaji wa maji mashinani ni moja ya miradi muhimu iliyoathiriwa.

“Tumeshuhudia miradi ambayo imebadilisha maisha ya wakazi wa mashinani kupitia hazina hii. Huduma ya maji imegatuliwa, kwa hivyo serikali ya kaunti inafaa kupiga jeki miradi ya serikali kuu,” Bw Nabulindo akaongeza.

Kwa moto uo huo, Mbunge wa Ganze Kazungu Tungule, ambaye pia ni mwanachama wa kamati hiyo, amelaumu kaunti kwa kukosa kufanya jambo kuhusiana na miradi iliyokwama vijijini.

Kamati hiyo imepinga kuhamishwa kwa jukumu la utathmini wa mamlaka ya maendeleo kwa kaunti ikisema serikali ya kitaifa imeunda mifumo ya kukagua miradi na imekuwa ikifanikiwa katika hili.

Mbunge wa Kajiado Mashariki Kakuta Mai Mai ameomba serikali isambaze pesa kufufua miradi ya maji iliyokwama katika eneobunge lake.

“Tunaomba serikali ikumbuke miradi iliyokwama wakati itaachilia pesa za malimbiliko ya madeni kama alivyosema Rais William Ruto alipokuwa akihutubia taifa katika Bunge la Kitaifa juma lililopita,” alisema Bw Mai Mai.

Mamlaka ya Maendeleo ya Ewaso Nyiro Kusini (ENSDA) imekamilisha miradi michache ikiwemo ile ya ujenzi wa bwawa la Sh25 milioni katika Kaunti ya Kajiado.

ENSDA ilikadiria bajeti ya mabwawa matatu na visima kumi katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024 kaendeleza kaunti mbili.

Afisa Mkuu wa ENSDA Ngala Oloitiptip alisema bwawa la Paranai lililoko Kajiado Mashariki linaweza kusambaza maji kwa familia 2,000 na angalau mifugo 20,000.

Bwawa la Embolioi la thamani ya Sh16 milioni, ni miongoni mwa miradi iliyotambuliwa kuwa muhimu. Kufikia sasa halijakamilika huku ujenzi ukiwa katika hatua ya asilimia 70.

Hii imesababisha wakazi wa eneo hili kutembea umbali wa kilomita 10 kuteka maji wakitumia punda.

“Licha ya changamoto za kifedha, tumekamilisha miradi ambayo imebadilisha maisha ya maelfu ya wakazi katika Kaunti za Kajiado na Narok. Tunaomba serikali ya kitaifa itume fedha zaidi ili kukamilisha miradi,” alisema Bw Ngala.

Kajiado ni moja ya kaunti ambazo zinaathiriwa vibaya na ukosefu wa maji katika maeneo ya miji na mashinani.

Maji yaliyofunguliwa katika shamba mojawapo Naroosura. Wakulima huwa na ratiba ya unyunyizaji maji ili kupuka mgogoro na pia kuhifadhi chemchemi ya Enkong’u Enkare. Picha|Labaan Shabaan