Kanuni mpya za kudhibiti tabia mbaya katika sekta ya matatu kulinda abiria
SERIKALI ya Kaunti ya Nakuru imezindua Kanuni za Maadili ya uchukuzi wa umma ili kuhakikisha mfumo wa uchukuzi wa umma eneo hilo ni salama, faafu na hauna aina yoyote ya dhuluma.
Haya yanajiri huku uongozi wa Kaunti hiyo ukitangaza kuwa umedhamiria kudhibiti unyanyasaji wa kingono unaozingira sekta hiyo.
Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu wa kaunti, Bw Michael Kamau alisema kanuni hizo zilibuniwa kupitia mashauriano na taasisi za utafiti na wadau, zinalenga vyama vya matatu, wafanyakazi katika sekta hiyo na washirika ili kuwa na mfumo salama wa kijamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kanuni hizo, Bw Kamau alibainisha kuwa mfumo wa uchukuzi wa umma nchini umekumbwa na matatizo kadhaa yakijumuisha dhuluma za kimapenzi zikilenga wanawake na kusisitiza kuwa serikali ya Kaunti imejitolea kuhakikisha kuwa sekta hiyo ni salama, nafuu na ni ya kutegemewa na wakazi wa Nakuru.
Wizara hiyo ya uchukuzi ilifafanua kuwa kanuni hizo zitatumika kwa wahudumu wote wa magari katika sekta ya uchukuzi wa umma, ambapo kanuni hizo zilitarajiwa kurejesha utulivu na kuimarisha ubora wa huduma katika sekta ya Matatu na sekta nyingine za usafiri wa umma Nakuru.
Bw Kamau aliongeza kuwa, kanuni hizo hazitatumika tu miongoni mwa sekta ya matatu bali pia kwa tuk-tuk, waendesha bodaboda na aina zote za usafiri wa umma.
‘Kanuni hizi ni pana kwani maendeleo yake yalihusisha ushirikishaji mkubwa wa umma na mashauriano na washikadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na serikali ya Kaunti, Huduma ya Kitaifa ya Polisi, na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA),’ akaeleza Bw Kamau.
Kulingana na kanuni hiyo, dhuluma ya kimapenzi hujidhihirisha kwa njia ya kuguswa bila idhini, kugusana kimwili waziwazi, maoni au utani unaochochea ngono, picha au mabango yanayoonyesha ngono waziwazi au matusi.
Kanuni hiyo inatwika majukumu kwa wadau katika sekta ya uchukuzi wa umma ikiwa ni pamoja na NTSA, wamiliki wa matatu, maafisa wa vyama vya matatu, wafanyakazi (madereva na makondakta) na hata abiria.
Kando na hayo, Bw Kamau alifafanua kwamba Kanuni hizo ziliegemezwa katika kanuni muhimu kama vile kukuza sekta ya usafiri, kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa kupitia uhifadhi wa mazingira, kuhakikisha heshima na kutobaguliwa kwa wateja na kujitolea kwa ustawi wa makundi hatari.
Ili kukuza ufahamu na uelewa wa Kanuni, wizara hiyo ilisema mikutano ya uhamasishaji itaandaliwa na wahudumu wa matatu, ikionyesha umuhimu wake kwa wakazi wa Nakuru na wahudumu wenyewe.
Kwa mujibu wa Kanuni, madereva na makondakta wanatakiwa kutofanya kazi wakiwa walevi au kutoa vitisho au kushiriki katika shughuli za vurugu zinazolenga kuwaathiri walengwa