Kaunti yaagizwa kulipa wamiliki wa ardhi Sh12.6 milioni
SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeagizwa kulipa wamiliki wawili wa ardhi Sh12.6 milioni ikiwa ni fidia kwa kuingiliwa kwa shamba lao kinyume cha sheria.
Jaji Stephen Kibunja wa mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Mombasa pia aliagiza kaunti ya Mombasa kuwalipa Aliakber Chakera na Fakhruddin Chakera Sh100,000 kama fidia ya jumla.
Mahakama pia ilitoa uamuzi ya kuwa vitendo vilivyonuiwa dhidi ya ardhi ya Bw Aliakber and Fakhruddin iliyoko kisiwani Mombasa ni kinyume cha sheria na kupita nguvu za kisheria na ilikuwa ni kuingia humo bila ruhusa na kuhitilafiana na mali ya kibinasfi.
“Upande pekee ambao unadai umiliki wa ardhi na ambao umetoa ushahidi ni walalamishi (Aliakber na Fakhruddin), cheti cha umiliki wa ardhi walichotoa kama ushahidi hakijapingwa,” alisema Jaji Kibunja.
Jaji Kibunja alisema kuwa waweka kesi walikuwa wamethibitisha madai yao dhidi ya serikali ya kaunti kama inavyostahili kisheria na wana haki ya maombi yao kukubaliwa.
Mahakama ilisema kuwa hata ingawa serikali ya kaunti ilidai kuwa mmiliki wa ardhi hiyo, haikutoa ushahidi wowote kuunga mkono dai hilo lililowasilishwa mahakamani.
“Mshtakiwa hakutoa ushahidi wowote kuunga mkono dai lao la umiliki wa ardhi. Stakabadhi zao za kesi kuwa taarifa ya kile wanachodai bila ushahidi haiwezi kuchukuliwa kama ithibati ya kilichomo humo,” alisema Jaji Kibunja.
Aidha, alisema kuwa japo serikali ya kaunti ilidai kuwa walalamishi walikuwa wamepata cheti cha ardhi kwa njia isiyostahili, haikuwa imetoa ushahidi, licha ya kupewa nafasi ya kuweka stakabadhi, taarifa za mashahidi na kuweka ushahidi wakati wa kesi kusikizwa.
“Madai ya kaunti dhidi ya walalamishi kuhusiana na kupata umiliki wa ardhi hiyo na cheti yatabaki kuwa yasiyothibitishwa na kwamba cheti cha ardhi hakiwezi kupingwa,” alisema Jaji Kibunja.
Kulingana na walalamishi, wao ndio wamiliki wa ardhi waliosajiliwa na kwamba kupitia mababu zao wamekuwa wamiliki tangu mwaka wa 1960 na kuweka nyumba ambazo zimekodishwa na wapangaji wanaofanya biashara tofauti tofauti.
Walalamishi walisema kuwa mnamo Januari 29, 2015, baadhi ya wafanyikazi wa serikali ya Kaunti ya Mombasa kutoka kwa Idara ya Ardhi waliingia kwa ardhi hiyo bila idhini na kutishia kuwatoa wapangaji na kubomoa nyumba zao.
Waliongeza kusema kuwa serikali ya kaunti, kinyume cha sheria ilitengeneza barabara ambayo haikuwa imekaguliwa ambayo ilipitia kwa ardhi yao (walalamishi) na kwamba serikali ya kaunti iliwapotosha wapangaji wengine wasilipe kodi.
Serikali ya Kaunti ya Mombasa ilikuwa imepinga kesi ya walalamishi ikikanusha kuingia kwa ardhi hiyo kinyume cha sheria, ubomozi au kutimuliwa kwa waliomo humo.