Habari za Kaunti

Mkasa wa moto waachia wafanyabiashara wa soko la Toi jijini Nairobi hasara ya mamilioni

Na FRIDAH OKACHI August 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAFANYABISHARA zaidi ya 1,500 wamepata hasara ya mamilioni ya pesa katika soko la Toi jijini Nairobi kutokana na mkasa wa moto ulioanza alfajiri ya Jumamosi ya Agosti 3, 2024.

Mwenyekiti wa soko hilo Kenneth Jomba alikadiria hasara ya Sh750,000 baada ya nguo anazouza kuteketea.

Bw Jomba alikuwa na matumaini ya kufungua kazi yake ya kuuza nguo Jumamosi kama kawaida, japo akapigiwa simu saa kumi asubuhi na mlinzi wa soko hilo kuwa kuna mkasa wa moto.

“Nilipokea simu dakika mbili kabla ya saa kumi ambayo ilinifahamisha soko linateketea. Kufika hapa ilikuwa mwendo wa saa kumi na dakika 23 na kufahamu kuwa nimeathiriwa pakubwa,” alisema Bw Jomba.

“Jana nilichukua nguo bale nne kwa msambazaji wangu Gikomba…”akaongeza kabla ya kulemewa na hisia na kushindwa kabisa kuongea kwa muda.

Soko hilo ambalo huwa na karibu wafanyabiashara 3,000, huwa limegawanywa katika sehemu 10. Hii ni kulingana na biashara mbalimbali kama vile za uuzaji wa nguo, vyakula, bidhaa za useremala na viatu.

Bw Jomba alisema kuwa moto huo ulianzia sehemu ambayo huuziwa kuni na ukasambaa kwa kasi.

“Moto ulianza kule chini sehemu ambayo kuni zinauziwa. Kibanda changu kipo katika eneo la Section B, karibu na Shule ya Msingi ya Toi ambayo pia imeathirika kwa kiasi kidogo na sikuweza kuokoa chochote,” aliongeza.

Mwenyekiti huyo alilalamikia kupata hasara chini ya mwaka mmoja licha ya kuchukua mkopo kwenye benki kwa lengo la kuinua biashara yake mwaka huu.

“Mwaka jana mwezi Juni, soko hili liliteketea. Wengi wetu tulichukua mkopo ili kufanya biashara. Mimi mapema mwaka huu nilichukua mkopo wa Sh250,000 kutoka benki na hawataelewa kuwa bidhaa nilizokuwa nikiuza zimeteketea,” alikamilisha.

Chifu wa eneo la Woodley, Nehemiah Amwocha, alithibitisha kuwa wafanyabiashara watatu na mtoto mmoja walipoteza maisha yao walipokuwa wakiokoa mali yao.

“Wanne hao, walifika katika eneo la mkasa kuokoa mali yao. Lakini inaonekana walizidiwa na moto na moshi wakiwa kwenye nyumba almaarufu store,” alisema Bw Amwocha.

Mkurugenzi wa Masoko ya Kaunti ya Nairobi, Joyce Kyengo, alisema walifika katika eneo la tukio kudhibiti moto huo.

“Tulipata taarifa kuwa moto huo ulisababishwa na hitilafu za umeme kwenye kibanda kinachouza kuni na kuanza kusambaa. Maafisa wa kuzima moto walifika kwa wakati uliofaa kudhibiti moto huo,” alibainisha Bi Kyengo.