Habari za Kaunti

Nakuru kutumia sehemu ya bajeti ya Sh6.5 bilioni kukarabati mochari

Na ERIC MATARA August 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kaunti ya Nakuru itatumia sehemu ya Sh6.5 bilioni kwenye bajeti yake katika sekta ya afya kukarabati mochari kwenye hospitali mbalimbali katika gatuzi hilo.  

Waziri wa Afya Rosyln Mungai amesema kuwa vyumba vya kuhifadhia maiti katika hospitali mbalimbali vimetelekezwa ila sasa vitakarabatiwa na kuongezewa vifaa vya kuhifadhi miili.

Bi Mungai amesema kati ya hospitali ambazo zinalengwa ni Nakuru Level Five, Molo, Elburgon na Olenguruone.

Mnamo Jumatatu wiki jana, hospitali ya Olenguruone ilipokea majokofu 12 ya kuhifadhi miili na rafu ya kuwekea miili ambayo tayari imeandaliwa tayari kwa mazishi.

Kaunti inalenga kupandisha hadhi ya mochari katika Hospitali ya Molo ambayo hupokea miili kutokana na ajali za mara kwa mara kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Chumba hicho cha kuhifadhi maiti kina nafasi kidogo ya kuhifadhi miili na miili mingine imekuwa ikipelekwa katika Hospitali ya Nakuru Level 5 na pia ile ya Kaunti ya Nakuru ambayo ilianzishwa miaka ya 60.

Mochari katika Hospitali ya Nakuru Level Five pia itapandishwa hadhi baada ya ukarabati huo ili ihudumie vyema kaunti za Nakuru, Kericho, Baringo, Nyandarua, Samburu na Narok.

Mochari ya Hospitali ya Nakuru Level 5 inaweza kubeba miili 100 na zaidi lakini imekuwa ikikabiliwa na msongamano kutokana na miili ambayo imetelekezwa na haijachukuliwa na wenyewe.

Usimamizi wa mochari kwenye Hospitali ya Nakuru Level 5 umekuwa ukizika zaidi ya miili 25 baada ya kila miezi sita na imekuwa ikisema hilo ndilo limekuwa tatizo kuu kwa mochari hiyo.

“Baadhi ya familia huwaleta watoto wao hospitalini kisha kukataa kuchukua miili yao wakiaga dunia. Huwa tunalazimika kuhifadhi miili yao kama mingine kwa muda wa miezi sita kabla ya kuizika,” akasema Afisa wa Afya ya Umma wa kaunti hiyo George Gachomba.

“Gharama ya kuhifadhi miili hii kwenye mochari ni ghali sana na wengi nao hawataki kuja kutambua miili ya wapendwa wao. Serikali ya kaunti imekuwa ikilipa bili kubwa ya umeme unaotumika katika kuhifadhi miili hiyo,” akaongeza.

Kando na mochari, Kaunti ya Nakuru pia inakabiliwa na uhaba wa makaburi hasa maeneo ya Nakuru Kusini na Kaskazini, Njoro na mjini Naivasha.

Makaburi katika maeneo haya tayari yamejaa huku baadhi ya makuburi yakichimbwa hadi katika njia au ile iliyotumika hapo awali ikiongezewa miili.