Polisi wakamata washukiwa 15 wa ‘Jeshi Jinga’
POLISI katika kaunti ya Kakamega wanazuilia vijana 15 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa genge la wahalifu linaloitwa Jeshi Jinga, ambalo limekuwa likihangaisha wakazi katika maeneo ya Mumias Mashariki, Mumias Magharibi, Navakholo na Lurambi.
Maafisa wa usalama pia wamerejesha ng’ombe 15 na mbuzi mmoja ambao walikuwa wameibwa pamoja na lori aina ya Canter ambalo linadaiwa kutumiwa kusafirisha wanyama hao.
Naibu Kamanda wa polisi Kaunti ya Mumias Mashariki, Beatrice Odiro, alisema washukiwa walikamatwa katika operesheni ya siku tatu kusaka wezi wa mifugo na kukabiliana na wahalifu.
Vijana hao walikamatwa katika vijiji vya Kamashia na Ekero katika kaunti ndogo ya Mumias Mashariki wakiwa na ng’ombe 15 na mbuzi mmoja wanaodaiwa kuibwa kutoka kwa wakazi wa maeneo hayo.
Wakazi wa Mumias wamekuwa na wasiwasi kufuatia kuongezeka kwa wizi wa mifugo eneo hilo, ambapo familia nyingi zimekuwa zikipata hasara.
Wakazi walisema kuwa visa vya uhalifu, ikiwa ni pamoja na wizi wa mifugo vimeongezeka katika kipindi cha hivi karibuni.