Usiporudisha Jumwa, umaarufu wa UDA Kilifi utazimika, Ruto aambiwa
HUENDA hatua ya Rais William Ruto kutomteua aliyekuwa waziri wa jinsia Aisha Jumwa, kwenye baraza lake jipya la mawaziri ikaathiri pakubwa umaarufu wa chama cha UDA katika Kaunti ya Kilifi.
Baadhi ya wanachama wa UDA Kilifi, sasa wanahisi kwamba Rais Ruto ameenda kinyume na matarajio yao ya Bi Jumwa kujumuishwa kikamilifu kwenye nafasi kuu za uongozi wa serikali ya Kenya Kwanza licha ya kuwa mstari wa mbele kupeperusha bendera ya kaunti hiyo.
Mshirikishi wa chama cha UDA katika Kaunti hiyo, Bw Moses Matano, alisema huenda uchaguzi wa viongozi wa UDA ambao ulikuwa ufanyike Kaunti hiyo hautafanyika tena baada ya Bi Jumwa kukosa kuteuliwa katika baraza la mawaziri.
“Tumeshangazwa sana kwa sababu zile shida Aisha amepitia ndani ya Kilifi Kaunti ni shida ambazo mtu yeyote mwenye roho nyepesi angeacha ushirika wake na Rais Ruto, lakini Bi Jumwa alisimama naye kidete na kuhakikisha anazoa kura za Kilifi kwa kueneza ajenda ya UDA, ” alisema Bw Matano.
Jumatano, Rais William Ruto, aliteua baraza la mawaziri katika awamu ya pili, akiwataja mawaziri wawili pekee kutoka Pwani, ambao ni Mabw Hassan Joho na Salim Mvurya. Uteuzi huo ulikosolewa, huku Rais akikashifiwa kwa kukosa kuzingatia usawa wa jinsia katika ugavi wa nafasi hizo za mawaziri kutoka eneo la Pwani.
Mchanganuzi wa siasa Kaunti ya Kilifi, Bw Frankiline Ndoro, alitaja hatua hiyo kama njama tu ya Rais Ruto kumeza ODM na kujizolea kura alizokosa katika uchaguzi uliopita.
“Hizi ni juhudi za Rais kushinda ile asilimia 30 ambayo ilikosa katika uchaguzi uliopita lakini ila anafaa ajue kuna asilimia karibu 35 ambayo haikujitokeza kupiga kura kwa hivyo, kuleta upinzani pekee katika serikali haitoshi na ndio maana unaona mchipuko wa vijana wanaojiita Gen-Z. Aidha walikiri kuwa Bw Raila Odinga atasalia kuwa yule yule mpenda maslahi na kigeugeu,” alisema Bw Ndoro.
Aliongeza, “Bw Raila atasalia kuwa yuleyule, hata ukiangalia hakuna hata mwanamke mmoja kutoka mrengo wa ODM ama Azimio amechaguliwa katika baraza hilo la mawaziri isipokuwa tu mabwanyenye wenye kufadhili chama cha ODM.”
Wakati huo huo, wanachama wake kwa waume, walielezea kuachwa njia panda kutokana na hatua hiyo ya Rais Ruto.
“Kama hakuna Bi Jumwa hakuna UDA huku Kilifi na tutaunda chama kingine maana tumekosa mwelekeo,” alisema Bw Ndoro.
Mara tu baada ya kujiunga na chama cha UDA , Bi Jumwa alitangaza nia yake ya kuwa gavana wa kaunti ya Kilifi kumrithi Bw Amason Jeffah Kingi ambaye sasa ni Spika wa Seneti lakini akapoteza kwa Bw Gideon Mung’aro.
Kutokana na ushirikiano wa karibu na Rais, alitajwa kuwa waziri wa utumishi wa umma, wizara hiyo baadaye iligawanywa katika sehemu mbili. Jumwa na kubaki kama waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi za Kitaifa hadi Julai 11, 2024.