Viongozi imani tele ushirika wa Ruto na Raila utafaidi Nyanza
VIONGOZI wa ODM Kaunti ya Kisumu wameonyesha imani kuwa Nyanza itanufaika kwa miradi ya maendeleo kutokana na muafaka uliotiwa saini na Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga mapema mwezi huu.
Kisumu ilionekana kuchezewa shere kwenye uteuzi ambao ulifanywa wa makatibu hivi majuzi na pia haina nafasi yoyote ya uwaziri. Aliyekuwa katibu katika wizara ya uchukuzi Alfred K’ombudo ambaye anatoka Kisumu aliondolewa kwenye wadhifa wake na kuteuliwa naibu balozi.
Aliyekuwa Mbunge wa Nyando Fred Outa ndiye afisa wa ngazi ya juu serikalini kutoka Kaunti ya Kisumu akiwa balozi wa Kenya Misri. Viongozi wengine ni wale ambao wamechanguliwa lakini wikendi, baadhi ya wanasiasa walisema lengo kuu ni maendeleo kwa wale ambao wamepata nafasi serikalini.
Mbunge wa Seme Dkt James Nyikal ambaye hivi majuzi aliteuliwa mwenyekiti wa Kamati ya Afya Bungeni, alisema kuwa Kisumu ipo pazuri kuvuna matunda ya Serikali Jumuishi sawa na maeneo mengine ya Nyanza.
“Tuombe mkataba huu udumu na dalili yake imeanza kuonekana kwa sababu sasa tunashikilia vyeo muhimu ndani ya serikali,” akasema Dkt Nyikal ambaye anahudumu muhula wake wa tatu bungeni
Alikuwa akiongea wikendi wakati alipozindua miradi ya maendeleo ambayo ipo chini ya afisi ya Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga.
“Uteuzi wa Regina Orege kama katibu katika wizara ya uchukuzi ni ishara kuwa eneo letu sasa lipo katika ngazi ya juu na linatambuliwa wakati mambo yanaamuliwa kitaifa,” akasema .
Mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron alisema kuwa kushirikishwa kwa ODM na kupokezwa nafasi za juu kwenye kamati za bunge ni hatua kubwa.
“Tumewaona wandani wa Raila wakipata nyadhifa za uongozi kwenye kamati muhimu kama bajeti, afya, leba, uchukuzi, viwanda na vyama vya ushirika. Hii ni ishara kuwa watu wetu wanatambuliwa,” akasema Bw Oron.
Aidha, Dkt Nyikal alisema ushirikiano huo umesababisha baadhi ya miradi ambayo ilikuwa imekwama ianze kufufuliwa huku akiwaomba wakazi wajisajili kwa Bima ya Kitaifa ya Afya (SHA).
“Hata reli ya SGR ambayo ilikuwa imekwama sasa imerejeshwa. Kuwekwa lami kwa barabara ya Muhoroni-Mamboleo pia kunaendelea. Mazungumzo yanaendelea kuhusu ujenzi wa bwawa la Koru-Soin ambalo litapunguza mafuriko Nyando,” akasema Dkt Nyikal.
Bi Odinga naye alisema utawala wa Rais Ruto umeonyesha nia nzuri kwa Nyanza na akawataka wananchi wauunge mkono ili miradi iendelee.
“Hii serikali ni yetu na watu wasiwadanganye kuwa tuko nje. Wenzetu ambao wamepewa vyeo lazima wahakikishe kuwa wanatumia vyeo hivyo kuyabadilisha maisha ya raia,” akasema Bi Odinga.