Afueni machifu waliotekwa na Al Shabaab siku 60 zilizopita wakiwaachiliwa
MACHIFU watano waliotekwa nyara na watu walioshukiwa kuwa Al-Shabaab, Mandera jana waliachiliwa baada ya kuzuiliwa kwa siku 60 nchini Somalia.
Waziri wa Usalama, Kipchumba Murkomen jana alisema maafisa hao wa utawala wako nchini. Watano hao ni machifu Mohamed Adawa, Mohamed Hassan, Abdi Hassan, Mohamed Noor Hache na naibu chifu Ibrahim Gabow. Ripoti za wazee ziliarifu watano hao walikuwa wakizuiliwa maeneo tofauti katika eneo la Jilib, Somalia.
Wazee hao wamekuwa Somalia kwa kipindi cha miezi miwili wakijadiliana na wapiganaji wa Al Shabaab. Jilib ni mji ambao upo chini ya uongozi wa Al Qaeda, kundi lenye itikadi kali ya dini ya Kiislamu ambalo linahusishwa na Al Shabaab.
Bw Murkomen alisema machifu hao waliachiliwa kutokana na juhudi za serikali kuu, ile ya Kaunti ya Mandera pamoja na wazee.
Kamishina wa Kaunti ya Mandera Henry Ochako naye alikataa kuthibitisha taarifa hizo akisema kuwa hajawaona machifu hao kwa hivyo, hawezi kuthibitisha iwapo wameachiliwa huru.
“Siwezi kuthibitisha au kukanusha habari hizo kwa sababu bado hatujawaona. Hadi pale ambao watakuwa upande wetu, siwezi kusema nimewaona,” akasema Bw Ochako.
Kama tu kamishina wa kaunti, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Robinson Ndiwa pia alikataa kuthibitisha habari hizo,
“Tumezisikia habari hizo nzuri lakini hadi pale watakuwa mikononi mwetu, siwezi kuthibitisha wamewaachiliwa,” akasema.
Katika mji wa Wargadud ambako machifu hao wanatoka, wanafamilia na marafiki walikusanyika baada ya kupokea habari hizo. Wakizungumza kwa sauti ya chini, wenyeji waliwasifu wazee ambao walishiriki mazungumzo ili machifu hao wawaachiliwe.
“Hapa huwa hatuzungumzi sana kuhusu Al Shabaab kwa sababu adui yupo hapa na unaweza kumalizwa kwa kuzungumza kuwahusu,” akasema mwenyeji mmoja ambaye hakutaka jina lake litambuliwe.
Kwa mujibu wa mwenyeji mwengine habari ya kuwaachiliwa kwa machifu hao ziliwasilishwa na mzee moja Jumapili asubuhi na ikatangazwa msikitini jioni.
Duru zinaarifu kuwa serikali ilihusika katika kuwaokoa machifu hao.
“Gavana wetu alitutembelea na ujumbe kutoka kwa serikali kuu na tuliamini kwa sababu mambo yametengenea,” duru zikaarifu.
Bila kutaja kiwango, duru hizo zilisema pesa hizo zilichangishwa na serikali ya kaunti na ile ya kitaifa.
Imetafsiriwa na Cecil Odongo