Atwoli amtaka Ruto abadilishe katiba ili miradi ya serikali isipigwe breki na mahakama
KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU), Francis Atwoli, sasa anamtaka Rais William Ruto kusaidia katika kufanikishwa kwa mabadiliko ya Katiba kuzuia watu fulani kutumia mahakama kusitisha utekelezaji wa miradi ya serikali.
Akiongea Jumapili, Bw Atwoli alisema hakubaliani na kipengele cha katiba ya sasa kinachoruhusu mtu yeyote kuwasilisha kesi mahakamani kupinga hata miradi ya serikali yenye manufaa kwa wananchi.
Bw Atwoli alieleza kuwa kutokana na vikwazo kama hivyo, huenda Rais Ruto akakamilisha muhala wake wa kwanza bila kufanikisha utekelezaji wa miradi yoyote mikuu ambayo aliratibu kwenye manifesto yake.
“Tutakusaidia lakini unakumbwa na vita kubwa zaidi. Kwanza utusaidie tubadilishe katiba ya sasa ili kuondoa vikwazo dhidi ya miradi mbalimbali ya serikali yako. Haiwezekani kwamba ukitaka kuleta mradi mzuri wa kusaidia raia watu fulani wanakimbia kortini na kuuzuia, ilhali ni mradi wa kitaifa,” akaeleza.
“Kwa hivyo, tunakuomba rais usaidie kufanikisha marekebisho ya Katiba ili kuondoa vikwazo kama hivi vinavyozuia utekelezaji wa miradi ya kitaifa,” Bw Atwoli akaongeza.
Katibu huyo Mkuu wa COTU alikuwa akihutubu Jumapili mbele ya Rais Ruto katika ibada ya Kanisa la Church of God katika Shule ya Msingi ya Ekambuli, eneo bunge la Khwisero, kaunti ya Kakamega.
Bw Atwoli ni miongoni mwa viongozi kutoka kaunti hiyo na maeneo mengine ya nchini waliandamana na kiongozi.
Ibada hiyo iliongozwa na kiongozi wa kanisa hilo nchini Askofu Mkuu James Obunde akisaidiwa na viongozi wengine.
Kauli ya Bw Atwoli imejiri siku chache baada ya Rais Ruto mwenyewe kuitaka Idara ya Mahakama kukoma kutoa maamuzi yanayositisha utekelezaji wa miradi mikuu ya serikali.
“Tunaheshimu uhuru wa mahakama lakini nawaomba majaji wetu wajizuie wanapotoa maamuzi kuhusu kesi zinazohusu miradi ya serikali. Hii ni kwa sababu miradi hii ni yenye manufaa kwa Wakenya walioipigia kura serikali hii kwa misingi ya manifesto yake,” Rais akasema Jumatatu, Novemba 4, 2024, alipohudhuria maadhimisho ya miaka 12 tangu kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu.
Baadhi ya miradi ya serikali ya kitaifa ambayo imeyumbishwa na maamuzi yanayotolewa na mahakama ni mradi w ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na ule wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenya (JKIA).