Habari za Kitaifa

Duale aagiza makato ya SHA ya madaktari yafanywe na Hazina ya Kitaifa

Na WACHIRA MWANGI, MISHI GONGO May 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Afya, Aden Duale, amefichua kwa mshangao jinsi wahudumu wa afya walio mstari wa mbele wanavyonyimwa huduma za afya wanazotoa kwa Wakenya kutokana na kuchelewa kwa serikali kuu na kaunti kuwasilisha michango yao kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).

Bw Duale ameitaka Hazina ya Kitaifa kuanza kukata michango ya SHA moja kwa moja kutoka mishahara, kuhakikisha kuwa madaktari na wahudumu wengine wa afya wanapata huduma za matibabu kwa wakati, jambo ambalo limekuwa shida tangu kuzinduliwa kwa mpango huo mpya wa afya.

“Ni ukatili na haikubaliki kwamba wanaotoa huduma za afya hawawezi kuzipata wao wenyewe wanapozihitaji. Sio SHA inayowazuia, ni mfumo,” alisema Bw Duale.

Alisema haya akihutubia wajumbe katika Kongamano la Kisayansi la Kila Mwaka la Chama cha Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU) lililofanyika katika hoteli ya Pride Inn Paradise huko Shanzu, Mombasa.

“Nitalifikisha pendekezo la kukatwa kwa michango ya SHA moja kwa moja kwa Hazina ya Kitaifa. Hatuwezi kujenga mfumo wa UHC (Afya kwa Wote) bila kulinda ustawi wa wahudumu wa afya,” aliongeza.

Kauli yake imejiri wakati wa hasira miongoni mwa madaktari wanaolalamikia kunyimwa huduma katika hospitali kubwa licha ya michango yao kuonekana kwenye mishahara yao.

Maafisa wa KMPDU walieleza kuwa madaktari wamekuwa wakikataliwa katika hospitali kuu kwa sababu kaunti zimechelewa kuwasilisha michango ya SHA.

Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, alikubaliana na pendekezo hilo akisema kuwa kukatwa kwa michango moja kwa moja kutakomesha malimbikizi ya madeni na kunyimwa huduma.

Masuala mengine yaliyotawala kongamano hilo ni pamoja na ukosefu wa ufadhili wa kutosha, mishahara kuchelewa, uhaba wa wahudumu wa afya, na pengo la mafunzo ya juu.

Katibu Mkuu wa KMPDU, Dkt Davji Atellah, alisema chama chao kimeahirisha mgomo uliopangwa kote nchini kwa muda wa wiki mbili ili kutoa nafasi kwa mazungumzo na serikali kuu na za kaunti.