Gachagua: Afisa wangu alipigwa risasi
KWA mara ya kwanza Naibu Rais Rigathi Gachagua amezungumzia kisa ambapo afisa mmoja katika afisi yake alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.
Bw Gachagua alilalamikia kile alichokitaja kama kuhangaisha kwa wasaidizi wake na wandani wake wa kisasa akisema hiyo ni sehemu ya njama ya kudhulumu “ilhali mimi ni Naibu Rais.”
Kwenye mahojiano na vyombo vya habari vinavyopeperusha habari kwa lugha ya Kikuyu mnamo Jumapili usiku, Agosti 4, 2024 Bw Gachagua alifichua kuwa afisa mmoja wa Shirika la Ujasusi Nchini (NIS) aliyemwajiri kupambana na kero ya pombe na mihadarati alipigwa risasi.
Lakini afisa huyo, ambaye Bw Gachagua hakumtaja jina, aliponea kifo kwa tundu la sindano kwa kupata jeraha begani.
“Katika jaribio la kunitisha, afisa huyo alifuatwa akitoka nyumbani kwake Kileleshwa na mtu aliyekuwa amebebwa katika boda boda, na akampiga risasi. Kwa neema za Mungu, risasi haikosa kichwa chake na kumpiga begani. Alikimbizwa Nairobi Hospital na risasi ikatolewa,” akaeleza.
Hata hivyo, Naibu Rais hakufichua siku au kipindi ambacho kisa hicho kilitokea.
Alisikitika kuwa kisa hicho hakikishughuliwa na asasi husika za kiusalama.
“Rais hakuwa na habari kuhusu tukio hili; ilinilazimu kumwarifu. Maafisa wakuu wa usalama walipoulizwa walianza kutatanika. Hadi wakati huu, mshambuliaji aliyetumwa kunitisha na wafanyakazi wangu hajafuatiliwa na suala hilo limenyamaziwa,” Bw Gachagua akaeleza.
Naibu Rais pia alizungumzia kwa mara ya kwanza hatua ya maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuwahoji wasaidizi wake watatu kuhusiana na madai kuwa walifadhili maandamano ya Gen Z.
Aidha, Bw Gachagua alielezea kisa ambapo Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru, almaarufu Meja Donk, alikabiliwa na magari 10 ya polisi eneo la Kenol, Murang’a na simu yake ikatwaliwa.
Aidha, simu ya Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya ilichukuliwa katika patashika hiyo.
Bw Gachagua alisema kuwa alimfahamisha Rais Ruto kuhusu matukio hayo na kumkumbusha ahadi aliyowapa Wakenya kwamba maafisa wa polisi hangetumiwa kuwahangaisha wanasiasa chini ya utawala wao.