Gachagua, Kiunjuri waendelea kulimana Mlimani baada ya ODM kuingia serikalini
MIEREKA ya kisiasa kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri sasa inaendelea kutokota Mlima Kenya hasa baada ya baadhi ya viongozi wa upinzani kuteuliwa serikalini.
Uhasama kati ya wanasiasa hao wawili umeongezeka mirengo yao sasa ikipanga mikutano tofauti ya kuhubiri umoja ili kuonyeshana ubabe wa kisiasa.
Bw Kiunjuri amekuwa akimlaumu Naibu Rais kwa kumhangaisha Rais William Ruto na kusababisha ainusuru serikali yake kupitia kuwateua wandani wa Raila Odinga serikalini.
Mrengo wa Bw Kiunjuri ambaye anahudumu muhula wake wa nne kama mbunge wa Laikipia Mashariki unapanga kuandaa kongamano kubwa la wanasiasa wa Mlima Kenya jijini Mombasa au Naivasha.
Mkutano huo utaamua mustakabali wa eneo hilo kisiasa kuelekea 2027 wakidai ‘kiburi’ cha Naibu Rais kimesababisha wapoteze thamani yao ndani ya utawala huu waliouchagua kwa kura nyingi mnamo 2022.
Kwa upande, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga ambaye amekuwa mtetezi sugu wa Naibu Rais na hata kudai kuwa anahangaishwa serikalini, amesema wataanza ziara rasmi ya kumpigia debe Bw Gachagua katika ngome yake ya Nyeri.
Hapo jana, Bw Kiunjuri, mwandani wa Rais Ruto alimkashifu Bw Gachagua akimtaja kama kiongozi dikteta ambaye nyota yake ya kisiasa haiwezi kung’aa na kutambisha Mlima Kenya popote.
“Sisi ambao tunaamini kwenye uongozi wa kweli na wenye uwazi Mlima Kenya tutaandaa kongamano letu Naivasha au Mombasa kuamua mustakabali wa kisiasa wa eneo letu,” akasema Bw Kinjuri.
Mbunge huyo kupitia chama chake cha TSP ni kati ya vinara wa muungano wa Kenya Kwanza na amekuwa mkosoaji mkubwa wa Naibu Rais. Bw Kiunjuri pia alishikilia nyadhifa za uwaziri kwenye utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
Baada ya kuhudumu kama mbunge wa Laikipia Mashariki (1997-2013), alihudumu kama waziri wa ugatuzi kuanzia (2015-2017) kisha waziri wa kilimo 2018 hadi Januari 2024 alipotimuliwa serikalini.
“Hakuna kitakachotuzia kuja pamoja dhidi ya kiongozi ambaye si muhimu kwa eneo letu. Viongozi 69 kati 75 wanasema mabaya kumhusu na wote hawa hawawezi kukosea, lazima atuheshimu,” akaongeza Bw Kiunjuri kwenye mahojiano na idhaa moja nchini.
“Wewe ndiye shida yetu. Kwa sasa jambo bora ni ujisaili nafasi na usake mbinu ya kusafisha makosa yako. Sina kisasi binafsi na Gachagua lakini mimi humjibu akinivamia,” akaongeza Bw Kiunjuri.
Mwezi uliopita, mbunge huyo alidai kuwa Naibu Rais alikuwa akifadhili maandamano yaliyokuwa yakishuhudiwa nchini na akasema aliwatuma wahuni 2,500 kuvuruga shughuli jijini Nairobi.
Bw Gachagua akionekana mwenye hamaki alimjibu na kumwaambia afunge kinywa au atoe ushahidi jinsi alivyohesabu wahuni hao na kujua idadi yao. Alimrejelea Bw Kiunjuri kama mwanasiasa mwenye njaa ambaye amekuwa akikodishwa na maadui wake ili kumdhalilisha kisiasa Mlima Kenya.
“Ni mtu wa kutumwa kisha kupewa pesa. Ameabisha Mlima Kenya kwa kudai tuliwatuma wahuni 25,000 na anastahili kutuambia vile aliwahesabu, jinsi alivyojua ni wa kabila letu na nambari ya magari yaliyowasafirisha? ” akasema Bw Gachagua.
Bw Kiunjuri jana aliongeza kuwa Rais Ruto hahitaji baraka za naibu wake tena kufika Mlima Kenya akisema Bw Gachagua alipoteza ushawishi wake kisiasa baada ya kukosa kuunda chama cha watu wa Mlimani kuelekea kura ya 2022
“Hakuna nyumba haina mtu na UDA si ya Gachagua. Wakati watu walikuwa wakiunda vyama na kuvitumia kudai mgao wao, yeye alikuwa akilala na kupeleka watu wetu UDA,” akasema Bw Kiunjuri akisema haogopi Naibu Rais na sasa anamakinikia kuwaunganisha wakazi wa Mlima Kenya.
Bw Kahiga naye anarindima ngoma ya Naibu Rais na amesema mkutano wa Nyeri ambao tarehe yake itatangazwa itakuwa mwanzo wa safari ya kumtunuku Bw Gachagua usemi katika siasa za eneo hilo.
“Tutatangaza tarahe na mahali kufikia mwisho wa mwezi huu. Viongozi wote wa Mlima Kenya wataalikwa ili tujadiliane jinsi ya kulinda maslahi yetu na mwelekeo ambao tutauchukua kisiasa,” akasema Bw Kahiga.
Huku Rais Ruto akionekana kuanza kuegemea ngome za kisiasa za Raila, naibu rais na Bw Kiunjuri wana kibarua kubwa cha kuhakikisha kuwa wanadumisha umoja wa mlima ili wawe na usemi katika kura ya 2027.