Gachagua kwenye kinywa cha mamba, kufika mbele ya ‘pilato’ jioni kujua hatima
NAIBU Rais Rigathi Gachagua leo atafahamu iwapo atanusurika au kupoteza, mchakato wa kuvuliwa wadhifa wake ukianza huku wabunge wakitarajiwa kupigia hoja ya kutokuwa na imani na uongozi wake.
Bunge la Kitaifa asubuhi hii itaanza kwa kujadili hoja ya kumng’oa Bw Gachagua ambayo iliwasilishwa wiki jana na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Hoja hiyo ilitiwa saini na wabunge 291 na iwapo itaungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge leo (233) kati 349 basi itapelekwa kwa Bunge la Seneti ndani ya siku mbili.
Hata hivyo, Bw Gachagua anaweza kunusurika tu iwapo wabunge 117 nao watapiga kura ya kupinga hoja hiyo hii leo.
Iwapo Naibu Rais atatimuliwa leo, basi hoja hiyo itapelekwa katika Bunge la Seneti ndani ya siku mbili. Huko theluthi mbili ya Maseneta wakiipitisha, basi Bw Gachagua atakuwa ameenda nyumbani.
Wikendi, Bw Gachagua akionekana mnyonge na mnyekekevu alishiriki ibada ambayo huenda ilikuwa ya mwisho katika makazi ya Naibu Rais kama wabunge watamtimua leo na seneti kuhalalisha hilo mnamo Alhamisi.
Wakati wa ibada hiyo mbunge huyo wa zamani wa Mathira alimwomba Rais William Ruto na wabunge msamaha, akisema ana majuto iwapo walikwaruzana wakati wa kuwahudumia Wakenya.
Pia kwa niaba ya mkewe Dorcas Rigathi, Naibu Rais aliomba msamaha iwapo miradi ambayo bibiye amekuwa akishiriki ya kumwuinua mtoto wa kiume, pia ilisababisha akosane na watu mbalimbali.
Mbele ya Bunge leo Jumanne, Naibu Rais atakuwa na mlima wa kuukwea katika mashtaka 11 ambayo yaliwasilishwa dhidi yake na Bw Mutuse wiki jana.
Ili kungátuliwa kwake, bunge linahitaji kudhibitisha tu kuwa kuna ushahidi wa kutosha kwenye shtaka moja na kulipitisha shtaka hilo. Hata hivyo, hatima ya Bw Gachagua itakuwa kwenye seneti ambayo inaweza kumwokoa au kummaliza wiki hii.
Maseneta wote 67 kisheria watapiga kura kwenye hoja dhidi ya Bw Gachagua ambapo anahitaji 22 aokolewe. Maseneta 45 wakiunga hoja hiyo basi naibu rais atakuwa ameondolewa kabisa kwenye wadhifa wake.
Katika kujitetea kwake, Bw Gachagua amemteua wakili maarufu na mbunge wa zamani Paul Muite kumtetea kuanzia saa 11 jioni hadi saa moja jioni. Hata hivyo, haijabainika iwapo atafika mwenyewe bungeni kujitetea au atawaruhusu mawakili wake wamfanyie kila kitu.
“Naibu Rais ana haki ya kufika mbele ya bunge kama mtu binafsi au kupitia mawakili wake au wote wafike wakati wa kuamuliwa kwa hoja dhidi yake,” akasema Spika.
“Vivyo hivyo mamlaka ya kumngóa Naibu Rais mamlakani au afisa yeyote ya serikali ipo kwa katiba. Bunge linatarajiwa kutimiza vigezo hivyo,” akaongeza Bw Wetangúla.
Katika kujitetea leo, Bw Gachagua atapambana na wadogo wake serikalini akiwemo Katibu kwenye Baraza la Mawaziri Mercy Njau, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Kusambaza Dawa Nchini (KEMSA) Andrew Mulwa.
Watatu hao waliwasilisha ushahidi wao katika Bunge la Kitaifa ambao walimshutumu Bw Gachagua kwa kukosa maadili ya uongozi na kuingilia kazi zao.
Bi Wanjau amesema Naibu Rais amekuwa akipinga maamuzi ya baraza la mawaziri ambako yeye ni mwanachama. Bw Sakaja naye amesema Bw Gachagua amekuwa akiwachochea wakazi wa Mlima Kenya dhidi ya utawala wake
Bw Mulwa naye amesema Bw Gachagua aliingilia mchakato wa utoaji tenda katika KEMSA ili kuhakikisha familia yake inanufaika. Orodha ya kampuni za Gachagua ambazo zilinufaika na tenda hizo za kaunti hizo inatarajiwa kuwekwa wazi bungeni na jinsi naibu rais alivyoshawishi tenda hizo.
Jaribio la Bw Gachagua kupata idhini ya korti nayo ziligonga mwamba jana baada ya mahakama kuamrisha kesi zote 19 ambazo ziliwasilishwa ziunganishwe kabla ya kusikizwa.
Ombi la kukubaliwa na kuunganishwa kwa kesi hizo lilikubaliwa na Bunge la Kitaifa pamoja na lile la Seneti.
Mnamo Ijumaa na Jumamosi, Wakenya walishiriki mikutano ya umma ambapo walitoa maoni yao kuhusu hoja hiyo. Bw Wetangúla anatarajiwa kuweka matokeo ya maoni hayo paruwanja leo na wengi wanasubiri kuona iwapo yanaoana na kile kilichosemwa na Wakenya.