Gachagua: Wewe Eric Wamumbi nilikusaidia kupata kiti na sasa unanipiga vita?
NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesema vita dhidi ya pombe haramu katika eneobunge la Mathira vinatatizwa na mbunge wa eneo hilo Eric Wamumbi.
Matamshi hayo yanaashiria kuzorota kwa uhusiano kati ya Naibu Rais na mbunge huyo baada ya wawili hao kutofautiana katika siasa za kitaifa.
Baada ya kuteuliwa mgombea mwenza wa Rais William Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Gachagua alikuwa na ushawishi mkubwa katika kuhakikisha Bw Wamumbi anapokezwa tiketi ya kumrithi katika eneobunge hilo.
Mbunge huyo hayupo kwenye kundi la wanasiasa kutoka Mlima Kenya ambao wanaegemea mrengo wa Bw Gachagua, akionekana kuwa katika tapo la wale walioko kambi ya Rais William Ruto.
Hapo jana, Bw Gachagua alisema Bw Wamumbi anamkosea heshima baada ya kuamrisha baa zilizokuwa zimefungwa, zifunguliwe na ziendeleze biashara kama zamani.
Wiki moja iliyopita inadaiwa Bw Wamumbi aliamrisha baa 400 Mathira zifunguliwe akisema alikuwa ameongea na mtu ambaye yupo katika afisi za juu serikalini.
Baa kadhaa Mathira zilikuwa zimefungwa kwa miezi minne iliyopita wakati ambapo serikali ilikuwa ikiendeleza vita dhidi ya pombe haramu.
“Haiaminiki kuwa mtu ambaye nilimsaidia kupata tikiti ya ubunge sasa amenigeuka na ananipiga vita. Alipata amri kutoka kwa nani ili baa za eneo hili zifunguliwe?
“Nawaambia msifuate amri yake kwa sababu sifahamu kikao chochote cha baraza la mawaziri ambapo kiliafikiwa baa zilizokuwa zimefungwa zirejelee biashara,” akasema Bw Gachagua.
Naibu Rais alikuwa akizungumza katika kanisa la Wamunyoro, kilomita chache kutoka nyumbani mwake Mathira, Kaunti ya Nyeri. Alishutumu mbunge huyo kwa kuwadanganya wamiliki wa baa kuwa alikuwa amezungumza na mtu mwenye ushawishi na anashikilia nafasi ya juu serikalini.
“Hayo maagizo yake ni haramu na ni sehemu ya mikakati ya wapinzani wangu kunionyesha madharau serikalini. Nawaambia wale ambao wamemtuma wakome au wanikabili kisiasa,” akaongeza.
Naibu Rais ambaye alihudumu kama mbunge wa Mathira kati ya 2017-2022 alisema yupo tayari kupoteza kazi yake ikiwa hilo litasababishwa na kumaliza pombe haramu ukanda wa Mlima Kenya.
“Nilipata kazi ya naibu rais miaka miwili iliyopita na si lazima nishikilie kazi hii milele. Kuongoza nchi ambayo pombe inawamaliza vijana si staha,” akasema.