Habari za Kitaifa

Gavana Nassir taabani baada ya kuhusishwa na kisa cha mwanablogu kubakwa Kisauni

Na BRIAN OCHARO September 24th, 2024 2 min read

GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, yumo taabani baada ya kuhusishwa katika kesi ambapo washukiwa wanne walishtakiwa kwa ubakaji na kumteka nyara mwanablogu.

Wanne hao, Bi Esther Muthoni John almaarufu kama Totoo, Bi Violet Adera almaarufu kama Vayoo, Bw Abdul Hassan Athman almaarufu kama Sindimba na Haji Babu Ndau Mohamed almaarufu kama Achkobe au Jay walifikishwa mbele ya mahakama ya Shanzu ambapo walikanusha mashtaka.

Kwa pamoja walishtakiwa kwa kosa la kula njama ya kutenda kosa, ambapo upande wa mashtaka ulidai kuwa, walikula njama ya kumteka nyara mwanablogu huyo aliyetambulika mahakamani kwa jina la BJK.

Serikali inadai kuwa wanne hao walitenda kosa hili mnamo Septemba 12, mahali pasipojulikana kwa pamoja na wengine ambao bado hawajakamatwa.

Mahakama ilielezwa kuwa, washukiwa hao walimteka nyara mwathiriwa katika eneo la Bamburi Jitegemee, Kaunti Ndogo Kisauni kabla kumpeleka mahali pasipojulikana ambapo walimpiga na kumlawiti kisha wakamwigiza kwenye gunia na kumwacha kichakani.

Bw Athman na Bw Mohamed pia walishtakiwa kwa kosa la kushambulia na kusababisha madhara halisi ya mwili.

Washukiwa wote wanne hata hivyo walikanusha mashtaka walipofika mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Shanzu, Bw Robert Mbogo.

Mahakama iliambiwa kuwa, Gavana Nassir na mamake ni miongoni mwa wale wanaotarajiwa kuandikisha taarifa kwa polisi huku uchunguzi kuhusu madai ya kutekwa nyara na kubakwa kwa mwanablogu huyo na kundi la watu.

Mahakama ilisikia kuwa, juhudi zaidi zinaendelea kurekodi taarifa hizi huku ikibainika pia kuwa huenda kukawa na majaribio ya kuwasaidia washukiwa wengine ambao wametajwa katika kitendo hicho cha kinyama kutoroka haki kwa kwenda mafichoni.

“Juhudi zaidi zinaendelea kuwakamata washukiwa waliosalia na kurekodi taarifa zikiwemo za Bw Nassir, mamake na maafisa wengine wakuu na mashuhuri wa kaunti ya Mombasa ambao tuna ripoti ya kijasusi kwamba wanasaidia baadhi ya washukiwa kutoroka,” Koplo Irene Karuga alisema.

Afisa huyo alisema anaweza tu kuthibitisha ripoti hii ya kijasusi kwa kuchanganua mawasiliano kati ya watu wanaohusishwa na kesi hiyo.

Bi Karuga alisema wapelelezi kwa sasa wanawasaka watu wasiopungua 15 ambao wanashukiwa kuhusika katika kisa hicho.

Mawakili wa washukiwa hao, Bw Jared Magolo na Bw Wycliffe Makasembo waliiomba mahakama kuwaachilia kwa dhamana kwa madai kuwa upande wa mashtaka haukutoa sababu za msingi za kuendelea kuwazuilia.

Mawakili hao walisema makazi ya wateja wao yanajulikana na kwamba wao ni Wakenya.

Wanne hao watasalia rumande hadi Alhamisi wakati mahakama itatoa uamuzi kuhusu ombi lao la dhamana.

Mahakama iliambiwa kuwa Bw Mohamed anaweza kutoroka iwapo ataachiliwa kwa dhamana kwa vile alipokamatwa, alikuwa katika eneo la Machakos kwenye basi lililokuwa likielekea mahali kusikojulikana baada ya kugundua washukiwa wenzake walikamatwa.