Habari za Kitaifa

HIVI PUNDE: Tume ya EACC yataka Oparanya anyimwe kiti cha uwaziri

Na CECIL ODONGO July 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi imeandikia Karani wa Bunge ikielezea wasiwasi wake kuhusu uteuzi wa gavana wa zamani wa Kakamega Wycliffe Oparanya kuwa waziri, ikisema anakabiliwa na kesi ya ufisadi.

Katika barua iliyoandikwa kwa Samwel Njoroge na Afisa Mkuu Mtendaji Twalib Mbarak, EACC inasema kwamba Bw Oparanya amekuwa akichunguzwa kwa makosa ya kiuchumi ikimaanisha kwamba uteuzi wake kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo Ndogo utakuwa unakiuka Kifungu nambari sita cha Katiba kuhusu maadili.

Bw Oparanya ni miongoni mwa vigogo wanne wa ODM walioteuliwa na Rais William Ruto wiki jana kujiunga na serikali yake aliyoitaja kuwa ‘jumuishi’ na inajiri baada ya maandamano makubwa ya vijana wa kizazi cha Gen Z yaliyomlazimu kuondoa Mswada wa Fedha 2024 pamoja na kuvunja baraza lake la mawaziri.

Bw Oparanya ni kati ya viongozi wanaoegemea mrengo wa Kinara wa Upinzani Raila Odinga ambao walibahatika kuteuliwa mawaziri.

Gavana huyo wa zamani anatarajiwa kufika mbele ya kamati ya kuwapiga msasa mawaziri wikendi hii na akiidhinishwa na bunge basi atahudumu katika wadhifa huo.

Hata hivyo, sasa anakabiliwa na giza mbele huku EACC ikiwa imemwaandikia Karani wa Bunge la Kitaifa ili asipigwe msasa kutokana na kesi ya ufisadi.

Kesi hiyo inahusisha ubadhirifu wa Sh28.9 milioni wakati ambapo alikuwa gavana wa Kakamega kati ya 2013-2022.

Naibu kiongozi huyo wa ODM amewahi kufika katika makao makuu ya EACC mara si moja na wake zake wawili kuhojiwa kuhusu matumizi mabaya ya pesa za umma alipokuwa nyapara wa kaunti.

Bw Oparanya amekuwa akimulikwa na EACC na ndiye waziri mteule pekee ambaye anaandamwa na suala la maadili huku wenzake 22 wakiwa hawajaandamwa au malalamishi kuwasilishwa dhidi yao.

Kando na Bw Oparanya wandani wengine wa Raila ambao walivuna na kuteuliwa mawaziri ni John Mbadi (Fedha), Opiyo Wandayi (Kawi), Hassan Joho (Madini) na Beatrice Ashakol (Jumuiya ya Afrika Mashariki).

Pia kigogo huyo wa ODM alionekana kuvuna kwa kuwa Mwanasheria Mkuu Mteule Dorcas Oduor anatoka katika ngome yake ya kisiasa ya Nyanza.