Habari za Kitaifa

Hospitali alikokufa Raila yazungumza

Na HILLARY KIMUYU October 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HOSPITALI ya Devamatha Kerala, kusini mwa India, ilithibitisha kuwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, ambaye aliaga dunia Jumatano, alianguka wakati wa matembezi ya asubuhi.

‘Tulifanya kila tuwezalo ikijumuisha CPR (ufufuo wa moyo na mishipa). Licha ya jitihada zetu, ikiwa ni pamoja na hatua nyingine za matibabu, hatukuweza kumwokoa. Tunasikitika sana kuwajulisha kwamba ameaga,”

‘Tunatuma rambirambi zetu kwa familia yake na watu wa Kenya,’ daktari wa magonjwa ya moyo Dkt Alphônš, kama alivyonukuliwa na Reuters, alisema.

Bw Odinga, mwanasiasa mashuhuri katika siasa za Kenya ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu na kuwania kiti cha urais mara tano bila mafanikio, alifariki akiwa na umri wa miaka 80 India.

Polisi wa eneo hilo na maafisa wa hospitali walithibitisha kuwa waziri mkuu huyo wa zamani alipatwa na mshtuko wa moyo. Afisa wa polisi wa India aliambia shirika la habari la AFP kwamba Bw Odinga alikuwa katika matembezi ya asubuhi, akiandamana na dadake, binti yake, daktari wa kibinafsi, na maafisa wa usalama wa India na Kenya, alipoanguka.

‘Alikimbizwa katika hospitali ya kibinafsi iliyo karibu, lakini alitangazwa kuwa amefariki,’ alisema Krishnan M, msimamizi wa ziada wa polisi Ernakulam, Kerala.

Gazeti la India la Mathrubhumi lilikuwa limeripoti kifo hicho hapo awali, na kuongeza kuwa Bw Odinga alikuwa akitibiwa katika jiji la Kochi jimboni humo.

Kulingana na kanda ya video iliyopeperushwa na Reuters, mwili wake ulionekana ukitolewa nje ya hospitali huku amefungwa kwa kitambaa kijani.

Akizungumza alipokuwa akihutubia taifa kutoka Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto alisema Kenya itaomboleza kwa kipindi cha siku saba ambapo shughuli zote rasmi zimesitishwa na bendera kote nchini, zikiwemo Ikulu, ofisi za serikali, kambi za kijeshi na balozi, kupeperushwa nusu mlingoti.

‘Nimetangaza kipindi cha siku saba cha maombolezo ya kitaifa, ambapo bendera ya taifa itapeperushwa nusu mlingoti katika Jamhuri ya Kenya na katika misheni zetu zote nje ya nchi. Kama ishara ya heshima, nimeahirisha shughuli zangu zote za umma na ninawaomba watumishi na viongozi wengine wote wa umma wafanye hivyo ili tujumuike na taifa katika kipindi hiki cha maombolezo na kutafakari kwa kina mchango wa Bw Odinga katika Tiafa letu,” Rais Ruto alisema