Idara ya Mahakama yalia Ruto anaikazia bajeti
IDARA ya Mahakama huenda ikashindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu ikidai kuwa ina upungufu wa Sh15 bilioni katika mwaka mpya wa kifedha.
Haya yanajiri licha ya ahadi za ufadhili wa ziada kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza.
Katika mwaka ujao wa fedha wa 2025/26, unaoanza Julai, Hazina ya Kitaifa imependekeza mgao wa kati ya Sh24.9 bilioni na Sh23.4 bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh1.5 bilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo dhidi ya hitaji la bajeti la mahakama la Sh40 bilioni.
Hii inailazimisha idara hiyo kupunguza bajeti yake, ikiwemo kuondoa majaji wakuu ofisini.
Upungufu huu wa bajeti, mahakama inaonya, utadhoofisha juhudi za kujenga vituo vingi vya mahakama, kuajiri watumishi zaidi wa mahakama, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika mifumo ya mahakama, kuboresha ustawi wa wafanyakazi na kuhudumia wananchi ipasavyo.
Hatua za kuimarisha usalama katika mahakama nchini kote hasa kufuatia mauaji ya hakimu wa mahakama ya Makadara Monica Kivuti mnamo Juni 2024 pia zitaathiriwa kutokana na uhaba wa pesa.
Hizi ni miongoni mwa hatua zilizopendekezwa katika mwongozo wa miaka 10 wa Jaji Mkuu Martha Koome wa Mabadiliko ya Kijamii kupitia Upatikanaji wa Haki (STAJ) uliopangwa hadi 2033.
“Mahakama imekuwa ikipokea chini ya nusu ya mahitaji yake ya kibajeti. Upungufu huu umeathiri pakubwa utekelezaji wa programu muhimu,” waraka wa mfumo wa matumizi unaojulikana kama ‘Bajeti ya Mahakama’ ilisoma.
Miongoni mwa hatua zitakazoathirika ni kuajiri wafanyikazi wa ziada na kushughulikia kesi zinazoendelea kuwakatiza tamaa Wakenya.
Kwa mujibu wa waraka huo, mrundiko wa kesi ni tatizo kuu na idadi ya kesi ambazo hazijashughulikiwa ziliongezeka kutoka 185,903 mwaka wa fedha 2022/23 hadi 187,370 mwaka wa fedha 2023/24.
“Hii inachangiwa na wingi wa kesi na hili hutokea kwa kuwa hatuna mahakama ya kutosha kushughulikia kesi hizo zote.”
Ili kutatua tatizo hilo, Jaji Mkuu ametangaza mipango ya kupanua huduma za upatanishi zilizoambatanishwa na mahakama kutoka vituo 62 vya sasa hadi 77.
Vituo hivyo 15 vya ziada vitahusisha kaunti za Lamu, Kwale, Samburu, Wajir, Mandera na Taita Taveta.
“Tangu kuzinduliwa kwa programu ya upatanishi iliyoambatanishwa na mahakama mwaka wa 2016, mahakama imepata maendeleo makubwa katika kuunganisha upatanishi katika mfumo rasmi wa haki kwani zaidi ya kesi 26,991 zimeshughulikiwa, huku zaidi ya kesi 24,464 zikikamilika,” alisema Jaji Koome.