Habari za Kitaifa

Jeshi sasa laachiliwa kupambana na waandamanaji kupitia kwa tangazo rasmi la Serikali

Na MWANDISHI WETU June 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imetangaza kuruhusu jeshi la KDF kusaidia kuleta utulivu nchini, katika siku ambayo imeshuhudia maandamano yaliyosababisha maafa, majeruhi, majengo ya Bunge kuvamiwa pamoja na uharibifu mkubwa katika miji mbali mbali nchini.

Tangazo hili limetolewa kupitia kwa Gazeti Rasmi la Serikali Jumanne jioni, likiwa limetiwa saini na Waziri wa Ulinzi Aden Duale.

Maandamano ya kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024 yalifanyika katika kaunti 34 ikiwemo Nairobi, Mombasa,Eldoret, Nakuru, Meru, Embu na yalishuhudia idadi kubwa, wengi wao wakiwa vijana chipukizi almaarufu Gen Z.

Mswada huo hata hivyo ulipitishwa na Bunge na unasubiri sahihi ya Rais William Ruto.

Kumwagwa kwa wanajeshi wa KDF ambao kikatiba hawahusiki katika usalama wa ndani isipokuwa nyakati maalum, kama vile kukabiliana na majangili katika Bonde la Ufa kunatarajiwa kupokea kwa hisia mseto, kwa sababu ya uzito wa amri hiyo.

Habari zaidi ni kadiri tunavyozipokea….