Habari za Kitaifa

Junet: Gachagua ni kama amekuwa ‘chifu’ wa Wamunyoro

Na SAMMY WAWERU January 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIKAO cha bunge Alhamisi kiligeuzwa kuwa uga wa kushambulia aliyekuwa naibu rais, Rigathi Gachagua, miezi michache baada ya kubanduliwa mamlakani.

Mashambulizi hayo yakiporomoshwa na kiongozi wa wengi Bungeni, Junet Mohammed, ambaye pia ni mbunge wa ODM, alidai Bw Gachagua sasa amegeuka kuwa ‘chifu’ wa eneo analotoka kufuatia misururu ya mikutano anayoandaa nyumbani kwake.

Naibu huyo wa rais wa zamani, aliyebanduliwa 2024, anatoka Kijiji cha Wamunyoro, eneobunge la Mathira, Nyeri.

Bw Junet alitoa matamshi hayo wabunge walipokuwa wakishiriki mjadala kupitisha mawaziri walioteuliwa na Rais William Ruto majuzi.

“Naona kuna mwingine tuliyembandua kama naibu wa rais (akimaanisha Rigathi Gachagua), amekuwa ‘chifu’ wa eneo analotoka kufuatia mikutano ya watu anayoandaa kwake,” alisema mbunge huyo wa Suna Mashariki.

Hata ingawa mjadala ulikuwa wa kupitisha mawaziri wateule; Mutahi Kagwe (Afya), William Kabogo (Habari, Mawasiliano na Teknolojia – ICT) na Lee Kinyanjui aliyeteuliwa kuongoza Wizara ya Biashara, Junet alikashifu baadhi ya viongozi serikalini wanaokosoa serikali wanayohudumu.

Alitumia jukwaa la kuunga mkono uteuzi wa mawaziri hao baada ya kualikwa na kiongozi wa wengi Kimani Ichungwah, kurusha makombora ya mashambulizi.

Akitumia mafumbo kulima Gachagua, Junet ambaye ni mwandani wa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, alivunja wabunge wenza mbavu akidai angependa sana kutembea eneo la Wamunyoro.

Mashambulizi ya mbunge huyo vilevile, yaliskika kuporomoshewa Waziri wa Umma Bw Justin Muturi ambaye majuzi alilalamikia Idara ya Ujasusi (NIS) kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Noordin Haji kuteka nyara mwanawe mwaka uliopita.

“Ikiwa unataka kuhudumia watu wa eneo unalotoka, rejea huko. Ukiwa waziri, wewe ni kiongozi wa Wakenya wote,” Bw Junet alielezea, kauli hiyo ikiashiria kuwa onyo kwa mawaziri wateule endapo watajitosa kwenye siasa za kukosoa serikali.

ODM imekuwa ikishirikiana na serikali ya Rais Ruto, hasa baada ya Bw Raila Odinga kutangaza kuzika tofauti zake kisiasa na kiongozi wa nchi mwaka uliopita, 2024.

Kuhusu dai la Gachagua kugeuka kuwa ‘chifu’, mbunge wa Mathira, Eric Wamumbi alifafanua kwamba eneo la Wamunyoro lina chifu halisi.

“Ningependa kuarifu kiongozi wa wachache kuwa eneo la Wamunyoro lina chifu wake anayefanya kazi nzuri sana,” Wamumbi aliambia bunge, akisababisha wabunge kuangua kicheko.

Wabunge wakiwa bungeni, sheria za bunge zinawaruhusu kushambuliana kimaneno japo kwa heshima.