Habari za Kitaifa

Kalonzo ajitawaza kiongozi wa upinzani

Na CECIL ODONGO August 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka Jumanne, Agosti 27, 2024 alijitawaza kama kiongozi wa upinzani nchini baada ya Raila Odinga kuzindua rasmi kampeni za kutwaa uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AUC).

Jumanne, Rais William Ruto aliongoza nchi na Marais watatu wa ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) kuzindua rasmi azma ya Raila kuelekea kura hiyo ya AUC ambayo itafanyika Februari 2025.

Bw Musyoka, na vinara wenzake katika Azimio la Umoja Martha Karua na Eugene Wamalwa pamoja na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta walisusia hafla ya uzinduzi wa azma ya Raila AUC.

Kinara huyo wa ODM amekuwa na uhasama na wenzake ndani ya muungano wa Azimio, baada ya kuamua kufanya kazi na serikali.

Hii ni baada ya wandani wake wanne kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri la Rais William Ruto.

Jumanne, Bw Musyoka alisema hakuhudhuria hafla ya kuzindua azma ya Raila ya AUC kwa kuwa alitaka kudhihirisha kuwa yeye ndiye kiongozi wa upinzani nchini.

“Siko katika Ikulu kwa sababu nataka kuonyesha kuwa mimi ndiye kiongozi wa upinzani. Azimio haitavunjwa kwa sababu Raila ameagana na siasa za Kenya,” akasema Bw Musyoka, huku akibainisha wazi kuwa anaunga mkono azma ya Raila ya AUC.

“Niko tayari kuwa kiongozi rasmi wa upinzani. Hapa ndio upinzani upo japo tuna idadi ndogo katika bunge, tuna Wakenya upande wetu,” akaongeza Bw Musyoka, akiongeza kuwa Azimio bado itasalia kuwa imara bila Raila.

Makamu huyo wa rais wa zamani, Jumanne aliandaa kikao na wanahabari katika makao makuu ya Wiper wakati ambapo hotuba za kumuidhinisha Raila nazo zilikuwa zikitolewa Ikulu.

Aliandamana na Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene, Bw Wamalwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni.

“Hakuna pengo lolote la kisiasa kwa sababu Kalonzo ndiye mwanasiasa wa pili kwenye itifaki ndani ya Azimio. Iwapo unaunga Katiba ya Kenya na unataka itekelezwe, basi jiunge nasi,” akasema Bw Wamalwa.

Aidha, Bw Wamalwa alionekana kukejeli ODM akisema hatua ya wanasiasa wake kuteuliwa serikalini ilikuwa na nia ya kuokoa utawala wa Rais ambao ulikuwa unaelekea kusambaratishwa na Gen Z.

Wandani wa Bw Musyoka wamekuwa wakiona kuwa kuondoka kwa Raila katika siasa za Kenya kunampa kiongozi wao nafasi ya kujisuka vyema ili awanie urais 2027.

Kalonzo ameunga Raila katika azma yake ya kuongoza nchi mnamo 2013, 2017 na 2022 lakini waziri huyo mkuu wa zamani alilemewa debeni.